Mkutano wa 9 wa FOCAC unatarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 4 hadi 6, ambapo utafunguliwa na Rais Xi Jinping wa China. Rais Xi Jinping atatoa hotuba ya ufunguzi itakayobainisha mwelekeo wa China katika kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Mkutano huo utahudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka zaidi ya nchi 40 kati ya 54 za Afrika. Miongoni mwa viongozi mashuhuri wanaotarajiwa kushiriki ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. António Guterres, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mhe. Moussa Faki, na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Akinwumi A. Adesina.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameteuliwa na Serikali ya China kuhutubia katika hafla ya ufunguzi, akiiwakilisha Kanda ya Afrika Mashariki. Kaulimbiu ya mkutano huo ni “Kushirikiana ili Kuendeleza Usasa na Kujenga Jamii Bora ya China na Afrika kwa Mustakabali wa Pamoja” (Joining Hands to Advance Modernization and Build a High-Level China-Africa Community with a Shared Future).

Katika mkutano huu wa wakuu wa nchi na Serikali kwa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation-FOCAC), Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwasilisha miradi minne muhimu kwa Serikali ya China, akiwa na lengo la kupata mikopo nafuu na msaada wa utekelezaji. Mkutano huu, ambao kwa zaidi ya miongo miwili umejikita katika kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi za Afrika na China.
Miradi inayotarajiwa kuwasilishwa na Rais Samia ni pamoja na ujenzi wa mtandao wa mawasiliano vijijini awamu ya pili, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400 awamu ya pili na ya tatu, ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi (VETA) awamu ya pili, na ujenzi wa barabara Zanzibar zenye urefu wa kilomita 277.
Haya yalisemwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu ziara ya Rais Samia nchini China.
Balozi Kombo alieleza kuwa Tanzania inatarajia kuwasilisha miradi mipya na ile ambayo haikuweza kutekelezwa kwenye mpango uliopita wa FOCAC kwa sababu mbalimbali, ili kupata fedha za mikopo nafuu na msaada kwa utekelezaji chini ya mpango kazi wa FOCAC 2025-2027.
Malengo ya Tanzania Kwenye Mkutano wa FOCAC
Balozi Kombo alitaja malengo matatu makuu ya ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano huo. Kwanza, ni kuimarisha na kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China, ambao mwaka huu umetimiza miaka 60.
Pili, kujadiliana na Serikali ya China kuhusu kuimarisha ushirikiano kwenye sekta za kipaumbele kama miundombinu, mifumo ya chakula, biashara, uwekezaji, ubadilishanaji wa ujuzi, upatikanaji wa nishati safi na salama, na kusaidia ujenzi wa uchumi wa kidijitali.
Lengo la tatu ni kuibua fursa mpya za ushirikiano kwa manufaa ya pande zote, kutangaza maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali katika sheria za sekta ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi.
Mkutano na Rais Xi Jinping na Makubaliano ya Reli ya TAZARA.
Rais Samia pia atafanya mkutano na Rais wa China, Xi Jinping, ambapo watajadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya mataifa yetu mawili. Aidha, watahudhuria hafla ya pamoja kutia saini makubaliano ya kuifufua Reli ya TAZARA.
Balozi Kombo aliongeza kuwa Rais Samia atafanya mazungumzo na kampuni za China ambazo zipo tayari kuwekeza kwa kiwango kikubwa na kufungua ofisi zao nchini Tanzania. Pia atakutana na viongozi wa kampuni kubwa za China katika hafla ya chakula cha jioni, lengo likiwa ni kuhamasisha uwekezaji zaidi nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, uwekezaji wa China nchini Tanzania umefikia Shilingi trilioni 30. Tangu kuanzishwa kwa FOCAC mwaka 2000, jukwaa hili limewezesha miradi mikubwa ya miundombinu barani Afrika, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, na uwekezaji katika sekta ya nishati.
