Rais Samia Akutana na Viongozi wa Kimataifa,Aeleza Mwelekeo wa Diplomasia ya Uchumi na Maendeleo ya Tanzania.

Scroll Down To Discover
Font size:

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, siku ya tarehe 15/01/2026 amekutana na Mabalozi, Makamishna Wakuu pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa katika mkutano wa kila mwaka wa kidiplomasia uliofanyika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma, ukiwa ni mkutano wa kwanza kufanyika katika jijini Dodoma.

Katika mkutano huo, Rais Samia amewakaribisha viongozi hao wa kidiplomasia na kuwatakia heri ya Mwaka Mpya 2026, akisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano kamili na mazingira salama katika utekelezaji wa majukumu yao nchini. Aidha, amewakaribisha Mabalozi na wawakilishi wapya waliojiunga na jumuiya ya kidiplomasia tangu mkutano uliopita.

Akizungumza kuhusu mazingira ya kimataifa, Rais Samia ameeleza kuwa dunia inaendelea kukumbwa na changamoto nyingi zikiwemo migogoro ya kisiasa, hali ngumu ya kiuchumi na athari za mabadiliko ya tabianchi. Katika mazingira hayo, amesisitiza kuwa Tanzania inaamini kwa dhati katika mazungumzo, ushirikiano na suluhisho za pamoja kupitia misingi ya kimataifa, na kueleza kuwa diplomasia ni nyenzo muhimu ya ustawi wa dunia.

Rais Samia pia ametumia fursa hiyo kuwakumbuka viongozi mashuhuri wa dunia waliofariki katika mwaka uliopita, akieleza kuwa mchango wao katika maendeleo ya binadamu utaendelea kukumbukwa. Aidha, amezipongeza nchi mbalimbali barani Afrika na duniani kwa kufanikisha chaguzi mbali mbali zilizofanyika na

mabadiliko ya madaraka kwa amani, akiwahakikishia kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na serikali mpya kuimarisha dira ya Umoja wa Afrika ya bara lenye mshikamano na ustawi.

Akizungumzia diplomasia ya uchumi, Rais Samia ameeleza kuwa imeendelea kuwa kiini cha sera ya mambo ya nje ya Tanzania, ikilenga kuvutia uwekezaji, kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, na kukuza sekta za kimkakati zitakazochochea ukuaji wa uchumi, ajira na maendeleo jumuishi. Akibainisha kuwa Serikali inaweka mkazo katika uchumi wa buluu na kijani, viwanda, usafiri na usafirishaji, teknolojia ya kidijitali pamoja na sekta ya madini ikiwemo gesi asilia, chuma na madini muhimu.

Rais Samia pia ameelezea mafanikio ya Tanzania katika uchaguzi wake wa saba wa kidemokrasia, ambapo asilimia karibu 44 ya wabunge ni wanawake na uchaguzi huo umegharamiwa kwa rasilimali za ndani pekee, hatua inayoonesha ukomavu wa taasisi na kujitegemea kwa kitaifa katika mchakato huo wa demokrasia. Hata hivyo, Mhe Rais amekiri kuwepo kwa changamoto za vurugu na machafuko siku ya uchaguzi na kuwa hatua zilizochukuliwa zililenga kulinda utulivu wa kikatiba na usalama wa raia pamoja na jumuiya ya kimataifa.

Kwa lengo la kuponya Taifa na kuliunganisha pamoja, Rais Samia ametaja hatua kadhaa zilizochukuliwa ikiwemo kuanzishwa kwa Wizara ya Vijana chini ya Ofisi ya Rais, kutoa msamaha kwa wafungwa 1,787 waliokuwa wanahusishwa na machafuko, kuunda Tume Huru ya Uchunguzi, pamoja na ahadi ya kuanzisha Tume ya Ukweli na Maridhiano kama sehemu ya mchakato wa Katiba Mpya.

Akizungumzia hali ya uchumi, Rais Samia ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazokua kwa kasi barani Afrika kwa ukuaji wa pato la Taifa wa karibu asilimia 6, mfumuko wa bei wa asilimia 3.3, na deni la Taifa himilivu lililosimamiwa vyema na kufikia uwiano wa asilimia 48.2 ya Pato la Taifa. Aidha, ameeleza kuwa Soko la Hisa la Dar es Salaam limepata ongezeko la thamani ya soko kwa asilimia 34.3, huku Tanzania ikiendelea kunufaika na viwango bora vya mikopo kutoka Moody’s na Fitch.

Rais Samia ameeleza kuwa hali hiyo chanya ya uchumi imesababisha usajili wa miradi mipya 927 ya uwekezaji yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 11.4 mwaka 2025, miradi inayotarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 162,895 kwa Watanzania. Aidha, amebainisha kuwa ushiriki wa wawekezaji wa ndani umeendelea kuimarika, jambo linaloonesha kuongezeka kwa imani ya Watanzania katika uchumi wao.

Katika sekta za uzalishaji, Rais Samia ameeleza kuwa kilimo kimeendelea kukua kwa uwiano wa kujitosheleza kwa chakula wa asilimia 120, huku sekta ya madini ikishuhudia ongezeko la uzalishaji kwa zaidi ya asilimia 48, ikichochewa na dhahabu, makaa ya mawe na madini ya ujenzi. Serikali pia imeendelea kuchukua hatua za kuhakikisha sehemu ya dhahabu inayozalishwa inauzwa Benki Kuu ili kuimarisha akiba ya fedha za kigeni nchini.

Sekta ya utalii pia imepata mafanikio makubwa, ambapo mapato yameongezeka hadi kufikia dola bilioni 4 mwaka 2025, huku Tanzania ikitangazwa kuwa Kituo Bora cha Safari Duniani katika Tuzo za World Travel Awards 2025. Aidha, Shirika la Ndege la Taifa (Air Tanzania) limeendelea kupanua mtandao wake wa safari ili kukuza utalii, biashara na muunganiko wa kikanda.

Rais Samia pia amebainisha kuwa mwaka huu Tanzania inaanza rasmi utekelezaji Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 (Dira 2050), inayolenga kukuza uchumi kupitia tija ya kilimo, viwanda na uongezaji thamani. Katika muktadha huo, ameeleza kuwa Serikali inaendelea na maandalizi ya mradi mkubwa wa gesi asilia wa dola bilioni 42, utakaoiweka Tanzania katika ramani ya nishati duniani.

Kuhusu miundombinu, Rais Samia amesema kuwa kazi inaendelea kukamilisha Reli ya Kisasa (SGR) na Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki litakalokamilika Julai 2026. Akisisitiza kuwa miradi hiyo, pamoja na Bwawa la Umeme la Julius Nyerere, ni injini za uchumi mpya wa Tanzania unaotegemea uongezaji thamani na mauzo ya nje.

Katika kuhitimisha, Rais Samia amewahakikishia Mabalozi na jumuiya ya kimataifa kuwa Tanzania inaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa uwekezaji, maendeleo ya rasilimali watu, afya, elimu na viwanda vya dawa, huku akitoa wito wa ushirikiano kwa washirika wa kimataifa katika kuijenga Tanzania kama kitovu cha biashara, nishati, afya na maendeleo endelevu barani Afrika.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook