TANZANIA NA CHINA ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI

Scroll Down To Discover
Font size:

Dar es Salaam — Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 10 Januari 2026 amekutana na kufanya mazungumzo rasmi na Mheshimiwa Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, katika Ikulu ya Dar es Salaam, kwa lengo la kuimarisha na kuendeleza uhusiano wa kimkakati wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Samia ameeleza dhamira thabiti ya Serikali ya Tanzania ya kuendeleza ushirikiano wa kimkakati na China, akisisitiza kuwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili umejengwa juu ya misingi ya urafiki wa kudumu, kuheshimiana na kunufaishana. Aidha, aliishukuru Serikali ya China kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Tanzania kwa miaka mingi.

Rais Dkt. Samia amesisitiza umuhimu wa kupanua wigo wa mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la China, kwa lengo la kuboresha mizania ya biashara kati ya nchi hizo mbili. Akibainisha pia haja ya kuendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji, sambamba na kukuza mahusiano ya kijamii na kiuchumi baina ya wananchi wa Tanzania na China.

Vilevile, Rais Dkt. Samia ameeleza dhamira ya Tanzania ya kufufua na kuimarisha uendeshaji wa Reli ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), pamoja na kukuza shughuli za kiuchumi zinazotegemea reli hiyo. Hatua hiyo inalenga kuongeza mchango wa TAZARA katika maendeleo ya kikanda, hususan katika kukuza biashara, usafirishaji na ujumuishaji wa masoko ya kikanda.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mheshimiwa Wang Yi, alisema Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imejizatiti kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania. Akisisitiza kuwa China inaunga mkono kikamilifu jitihada za maendeleo za Serikali na wananchi wa Tanzania.

Waziri Wang Yi ameeleza kuwa Reli ya TAZARA ni alama muhimu ya historia ya urafiki wa muda mrefu kati ya China na Tanzania, na akaeleza kuwa China iko tayari kushirikiana na Tanzania katika maboresho ya reli hiyo ili kuongeza ufanisi wake na mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi ya kikanda.

Aidha, Waziri Yi aliongeza kuwa China itaendelea kuwa mshirika muhimu wa Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya kipaumbele, ikiwemo miradi ya miundombinu, maji, nishati safi ya kupikia, pamoja na kutoa mikopo nafuu na misaada ya maendeleo kwa ajili ya ustawi wa wananchi.

Nchi zote mbili zilithibitisha dhamira yao ya pamoja ya kuendeleza uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na wa pande nyingi kwa manufaa ya pamoja.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook