RAIS SAMIA AZINDUA HOTELI YA JAZ ELITE AURORA, ATOA TASWIRA YA MAFANIKIO MAKUBWA YA SEKTA YA UTALII

Scroll Down To Discover
Font size:

Michamvi, Zanzibar — Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameizindua rasmi Hoteli ya Kitalii ya Jaz Elite Aurora iliyopo Michamvi, Zanzibar, na kueleza kuwa wakati Taifa linaadhimisha Miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, nchi inaendelea kushuhudia kwa vitendo matokeo chanya ya utekelezaji wa sera madhubuti za uwekezaji zilizochochea mapinduzi ya kweli ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa uwekezaji unaoendelea kufanyika nchini umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la Pato la Taifa, upanuzi wa fursa za ajira, pamoja na kuimarika kwa hali ya maisha ya wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Rais amesisitiza kuwa sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia uzalishaji na utoaji wa huduma. Akibainisha kuwa sekta hiyo imekua kwa kasi kubwa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, ambapo kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 imeajiri zaidi ya Watanzania milioni 2.5.

Aidha, Rais Dkt. Samia alisema kuwa idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi imeongezeka kwa kiwango kikubwa, kutoka watalii 1,409,800 mwaka 2020 hadi kufikia watalii 5,360,247 mwaka juzi, hatua inayoonesha mafanikio makubwa ya jitihada za Serikali katika kufufua, kuimarisha na kuitangaza Tanzania kama kituo kikuu cha utalii ndani na nje ya nchi.

Vilevile, idadi ya mawakala wa biashara za utalii imeongezeka kutoka 2,885 mwaka 2020 hadi 3,735 mwaka 2025, huku idadi ya waongoza watalii ikiongezeka kutoka 5,076 mwaka 2020 hadi kufikia 7,862 mwaka 2025. Sambamba na mafanikio hayo, mapato yatokanayo na sekta ya utalii yameongezeka na kufikia Dola za Marekani bilioni 4.2 katika kipindi cha miaka 2022 hadi 2025.

Akizungumzia mafanikio ya sekta ya utalii Zanzibar, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa idadi ya watalii wanaotembelea visiwa hivyo imeongezeka kutoka watalii 743,606 mwaka 2024 hadi kufikia 816,000 mwaka 2025, huku matarajio yakiwa ni kuendelea kuongezeka zaidi katika miaka ijayo.

Aidha, Mhe Rais amebainisha kuwa kufikia mwaka jana, hoteli zaidi ya 400 zilikuwa zimefunguliwa na zinaendelea kutoa huduma, hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo mchango wa sekta ya utalii katika Pato la Serikali umeendelea kuwa zaidi ya asilimia 30.

Rais Dkt. Samia amehitimisha kwa kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji ili kuimarisha zaidi sekta ya utalii na sekta nyingine za uzalishaji, kwa lengo la kuhakikisha ukuaji endelevu wa uchumi na ustawi wa wananchi wa Tanzania kwa ujumla.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook