Dar es Salaam — Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewapongeza kwa dhati wanamichezo mbalimbali wa Taifa kwa mafanikio yao katika mashindano ya kimataifa, akitaja mafanikio hayo kuwa ni ushahidi wa kupanda kwa viwango vya michezo nchini na heshima kubwa kwa Taifa.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 10 Januari, 2026, katika hafla ya kuwapongeza wanamichezo, Rais Dkt. Samia aliipongeza timu ya Taifa ya mpira wa miguu, Taifa Stars, pamoja na benchi lake la ufundi kwa kufuzu na kufika hatua ya 16 bora ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mwaka huu.

Rais ameeleza kuwa mafanikio hayo ni ya kihistoria na yanadhihirisha wazi kuwa soka la Tanzania limeendelea kupanda viwango barani Afrika. Amebainisha kuwa hatua hiyo ni ushahidi wa mabadiliko chanya yanayoendelea katika sekta ya michezo, hususan mpira wa miguu, na imerejesha imani mpya kwa Watanzania katika ushindani wa kimataifa.
Aidha, Rais Dkt. Samia ametambua mchango mkubwa wa marehemu katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Serikali na Chama cha Mapinduzi, akieleza kuwa alikuwa na uwezo wa kubeba majukumu mazito kwa weledi, busara na uaminifu mkubwa. Na kuwa ufanisi wake katika majukumu aliyokabidhiwa uliakisi dhamira ya kweli ya kulitumikia Taifa kwa vitendo.
Akigusia urithi wa uongozi aliouacha, Rais Samia amesisitiza kuwa moyo wa marehemu Jenista ulikuwa wa kujali maslahi mapana ya Taifa na ndio nguzo kuu ya kumbukumbu yake na kutoa wito kwa wabunge na viongozi wote kuiga mfano wake wa maadili, uwajibikaji na utumishi wenye tija kwa wananchi.
Aidha, Rais Dkt. Samia alionesha kuridhishwa na kiwango cha mchezo kilichooneshwa na Taifa Stars, akieleza kuwa kwa mara ya kwanza alitazama mechi ya timu hiyo kupitia runinga kuanzia mwanzo hadi mwisho, jambo lililodhihirisha ubora na ushindani wa hali ya juu uliokuwepo uwanjani.
Katika hotuba yake, Rais Samia pia mabadiliko ya hivi karibuni ya kiutendaji ndani ya Serikali, akieleza kuwa yamelenga kuilinda na kuiimarisha Tanzania katika mazingira ya siasa za kimataifa. Alisema uamuzi wa kumhamisha Profesa Palamagamba Kabudi kutoka Wizara ya Michezo na kumteua kufanya kazi Ikulu ni wa kimkakati, unaozingatia mwelekeo wa siasa za dunia, ambapo baadhi ya mataifa yana mtazamo chanya kwa Tanzania na mengine yana mtazamo hasi.

Rais ameeleza kuwa Ikulu inahitaji washauri wenye akili iliyopevuka, maarifa mapana, uzoefu mkubwa na uwezo mzuri wa kujieleza na kufafanua masuala ya Taifa kwa uelewa mpana wa ndani na nje ya nchi.
Katika hatua ya kuimarisha ushauri wa kitaalamu katika ngazi ya juu ya uongozi, Rais Dkt. Samia pia ameeleza kuwa amemteua aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdori Mpango, kuwa mshauri wake katika masuala ya uchumi. Aidha, aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameteuliwa kuwa mshauri katika masuala ya kijamii, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa Serikali katika kusimamia maendeleo ya Taifa.
Akizungumzia kwa ujumla maendeleo ya michezo nchini, Rais Dkt. Samia amesema ni dhahiri kuwa sekta ya michezo imepiga hatua kubwa katika kipindi cha hivi karibuni. Aliwapongeza wanamichezo na timu zote za Taifa kwa mafanikio yao, akitaja timu mbalimbali zilizoliwakilisha Taifa kwa heshima katika mashindano ya kimataifa.
Miongoni mwa timu zilizotajwa ni timu ya Taifa ya kriketi iliyofuzu kushiriki Kombe la Dunia linalofanyika nchini Namibia, pamoja na timu ya Taifa ya mpira wa miguu wa wanawake iliyoshiriki Kombe la Dunia nchini Ufilipino, hatua iliyotajwa kuwa mafanikio makubwa katika historia ya michezo ya Tanzania.
Aidha, Mhe Rais amewapongeza mabondia wa Tanzania waliotwaa mikanda ya kimataifa, pamoja na timu ya Taifa ya ngumi za ridhaa iliyojinyakulia jumla ya medali 18, zikiwemo medali moja ya dhahabu, medali nne za fedha na medali 13 za shaba, katika mashindano ya Kanda ya Tatu ya Afrika yaliyofanyika Nairobi, nchini Kenya.
Rais Dkt. Samia amehitimisha kwa kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza na kuweka mazingira bora kwa maendeleo ya michezo nchini, ili kukuza vipaji, kuimarisha ushindani wa kimataifa na kuliletea Taifa heshima zaidi kupitia michezo.





