Rais Samia Aongoza Taifa Kumuaga Hayati Jenista Joakim Mhagama

Scroll Down To Discover
Font size:

Dodoma, 13 Desemba 2025 Taifa limeingia katika majonzi makubwa kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Mhe. Jenista Joakim Mhagama. Kufuatia tukio tukio hilo lililogusa hisia za wengi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameongoza familia, viongozi wa kitaifa, wabunge pamoja na waombolezaji katika ibada ya kuaga mwili wa marehemu iliyofanyika katika Kanisa la Mwenyeheri Maria-Theresa Ledochowska, Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.

Akizungumza wakati wa ibada hiyo, Rais Dkt. Samia alieleza masikitiko makubwa ya kufuatia msiba huo mzito, akimwelezea marehemu Jenista Mhagama kama kiongozi jasiri, mwaminifu na mwenye heshima kubwa katika utumishi wa umma. Dkt Samia ameeleza kuwa marehemu alikuwa mlezi wa viongozi wengi ndani ya Bunge na Serikali, aliyelitumikia Taifa kwa moyo wa kujitoa, nidhamu, uadilifu na hofu ya Mungu.

Rais Samia pia amebainisha kuwa katika kipindi chote cha utumishi wake, marehemu Jenista alisimama imara kutetea haki, maendeleo na usawa wa wananchi, akionesha mfano wa uongozi unaoweka mbele maslahi ya Taifa kuliko maslahi binafsi. Ris Samia amesisitiza kuwa Taifa limepoteza kiongozi aliyekuwa nguzo muhimu katika kujenga misingi ya uwajibikaji na uadilifu katika uongozi wa umma.

Aidha, Rais Dkt. Samia ametambua mchango mkubwa wa marehemu katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Serikali na Chama cha Mapinduzi, akieleza kuwa alikuwa na uwezo wa kubeba majukumu mazito kwa weledi, busara na uaminifu mkubwa. Na kuwa ufanisi wake katika majukumu aliyokabidhiwa uliakisi dhamira ya kweli ya kulitumikia Taifa kwa vitendo.

Akigusia urithi wa uongozi aliouacha, Rais Samia amesisitiza kuwa moyo wa marehemu Jenista ulikuwa wa kujali maslahi mapana ya Taifa na ndio nguzo kuu ya kumbukumbu yake na kutoa wito kwa wabunge na viongozi wote kuiga mfano wake wa maadili, uwajibikaji na utumishi wenye tija kwa wananchi.

Halikadhalika, Rais Dkt. Samia amewataka viongozi nchini kuuenzi mchango wa marehemu kwa kuimarisha mshikamano wa kitaifa, kudumisha maadili ya uongozi na kuhakikisha kuwa utumishi wa umma unaendelea kulenga maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Katika hitimisho la hotuba yake, Rais Samia ametoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, wananchi wa Jimbo la Peramiho, Bunge na Taifa kwa ujumla. Akimuomba Mwenyezi Mungu awape faraja, nguvu na amani katika kipindi hiki kigumu, huku akiiombea roho ya marehemu Jenista Joakim Mhagama pumziko la amani ya milele.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook