Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezungumza na Wazee wa Jiji la Dar es Salaam na taifa kwa ujumla, akifafanua kwa kina kuhusu matukio ya Oktoba 29, 2025, athari zake, chanzo chake na mwelekeo wa serikali katika kulinda amani na umoja wa nchi.
Katika hotuba hiyo, Rais ameonesha masikitiko makubwa kutokana na vifo na madhara yaliyotokana na vurugu zilizotokea. Dkt Samia ametoa salamu za pole kwa familia zote zilizopoteza ndugu na watoto wao, akisisitiza kuwa maumivu hayo si ya familia husika pekee bali ni ya taifa zima. Dkt Samia pia ameeleza kuwa kupotea kwa Mtanzania mmoja ni pigo kwa Watanzania wote kwa sababu maisha ya watanzania wote yana thamani sawa.

Vurugu Zilizotokea sio Maandamano Halali
Rais amefafanua kuwa tukio la Oktoba 29 halikuakisi maandamano ya kikatiba, bali ni vurugu zilizoratibiwa kwa malengo maalum. Akitaja uharibifu mkubwa uliotokea, ikiwemo majengo ya serikali, miradi ya wananchi, biashara binafsi, vituo vya mafuta, magari ya serikali na vituo vya polisi vilivyochomwa au kuvamiwa.
Dkt Samia ameeleza kuwa mwenendo huo hauwezi kuelezewa kama maandamano ya kuwasilisha maoni. Akisisitiza kuwa maandamano halali hufuata utaratibu wa amani na polisi huwa wasindikizaji, huku malengo yake yakielezeka wazi kupitia mabango na ujumbe unaostahili.
Nguvu ya Dola Ilitumika Kulinda Usalama wa Taifa
Mhe Rais ameeleza kuwa serikali ilichukua hatua madhubuti kukabiliana na vurugu hizo, akielezea kuwa kiwango cha nguvu kilichotumika kilikuwa sawa kulingana na ukubwa wa tukio. Amefafanua kuwa serikali ina jukumu la msingi la kulinda wananchi, mipaka, mali na utulivu wa nchi. Kwa upande wa kimataifa, ameeeleza kuwa mataifa yote yenye mifumo ya dola imara hutumia nguvu ya kutosha pale ambapo usalama wa taifa unahatarishwa.
Vijana na Changamoto ya Uzalendo
Katika hotuba yake, Rais alielezea kwa masikitiko kuwa vijana wengi waliokuwa barabarani hawakushiriki kwa misingi ya madai halali ya maisha magumu kama ilivyodaiwa kwenye mitandao ya kijamii, bali walitumika na baadhi ya watu wenye maslahi ya kisiasa. Mhe Rais ameeleza kuwa baadhi ya vijana walilipwa, wengine walifuata mkumbo bila kuelewa madhumuni, na wengine walihadaiwa kwa ahadi za maisha mazuri baada ya vurugu hizo.
Rais ameeleza kuwa tukio hilo limeonesha mapungufu makubwa katika malezi ya uzalendo kwa vijana. Hivyo basi Serikali kupitia wizara mpya ya vijana imekusudia kufanya kazi mahususi katika kujenga uzalendo, uelewa wa masuala ya taifa na uwezo wa vijana kupambanua propaganda na misukumo ya kisiasa.

Uingiliaji wa Nje na Masuala ya Katiba Mpya
Mhe Rais pia ameweka wazi kuwa misukumo ya baadhi ya madai, ikiwemo hoja ya Katiba mpya, imekuwa ikiungwa mkono na wadau kutoka nje ambao, wamekuwa wakitoa mashinikizo bila kujali mifumo ya kiserikali na muktadha wa ndani ya Tanzania. Ameeleza kuwa hakuna aliyegomea nia ya kuanzisha mchakato wa Katiba, kwani tayari Tume ya Haki Jinai ilishawasilisha mapendekezo na mengi ya muda mfupi na ya kati ambayo yameanza kutekelezwa.
Kwa sasa, serikali inasubiri Tume ya kuchunguza vurugu hizo kukamilisha kazi yake ndani ya miezi mitatu. Na baada ya hapo, Tume ya Maridhiano itaundwa, ikifuatiwa na mchakato wa Katiba mpya. Mhe Rais amesisitiza kuwa Katiba haiwezi kuandikwa katika mazingira ya taharuki, misuguano au hisia kali, bali katika mazingira ya maridhiano na utulivu.
Dar es Salaam Iko Kwenye Kiini cha Uchumi, Hivyo Madhara Yaliyotokea Yalikuwa Makubwa Zaidi
Rais Samia pia ameeleza kuwa vurugu hizo ziliathiri kwa kiwango kikubwa Jiji la Dar es Salaam, jiji ambalo linachangia asilimia 17 ya Pato la Taifa na lenye watu zaidi ya milioni sita. Amefafanua kuwa kusimama kwa shughuli za Dar es Salaam kunamaanisha kusimama kwa shughuli za taifa zima. Kupanda kwa bei za bidhaa na usumbufu kwa wananchi ni ishara ya uzito wa madhara hayo.
Kwa mujibu wa tathmini ya awali, vurugu hizo zilikuwa sehemu ya mradi mpana wenye wafadhili na washirika kutoka ndani na nje ya nchi, uliolenga kutikisisha utawala halali na kujaribu kuangusha dola. Amebainisha kuwa vijana walitumiwa kama zana, huku wengine wakiwa hata hawajui dhumuni la matukio hayo
Wito kwa Viongozi wa Dini na Wananchi Kutetea Amani
Mhe Rais pia ametoa wito mahsusi kwa viongozi wa dini, akiwataka kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani badala ya kutumia fursa hii kueneza chuki, hisia za kidini au visingizio vinavyoweza kuvuruga nchi. Akiwakumbusha kuwa mamlaka yoyote ipo kwa muda maalumu na kwamba kutokumkubali kiongozi hakutoi ruksa ya kuhatarisha amani ya taifa.
Mwelekeo Mpya: Tume, Maridhiano na Hatua za Mageuzi
Mwisho, Mhe Rais ameeleza kuwa pamoja na changamoto zilizojitokeza, serikali itasimama imara kuilinda nchi, kuhakikisha uchunguzi unafanyika kwa weledi, na kuendeleza mchakato wa Katiba mpya baada ya utulivu kurejea. Akisisitiza kuwa hoja za wapinzani hazijakataliwa, lakini taratibu lazima zifuatwe na taifa liwe katika hali ya kutulia kabla ya kufanya maamuzi makubwa kama ya Katiba.





