RAIS SAMIA AZINDUA TUME HURU YA UCHUNGUZI WA MATUKIO YA UVUNJIFU WA AMANI YA UCHAGUZI MKUU 2025

Scroll Down To Discover
Font size:

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi Tume Huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025. Tume hiyo ameiunda tarehe 18 Novemba 2025 kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi ya mwaka 2023 (Sura ya 32), na amemkabidhi uenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, huku akiwa ameipa muda wa miezi mitatu kutekeleza majukumu yake.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Rais Dkt. Samia amewashukuru wajumbe wa Tume kwa kukubali jukumu hilo muhimu kwa maslahi ya Taifa na amesisitiza kuwa ana imani na uwezo wao wa kulitumia weledi, uadilifu na uzalendo katika utekelezaji wa jukumu hili nyeti.

Ameeleza kuwa Tume hiyo itapatiwa hadidu za rejea zitakazoiongoza kufanya uchunguzi wa kina kuhusu chanzo cha matukio hayo, mienendo ya wadau wa siasa na jamii, hatua ambazo zimechukuliwa kukabiliana na vurugu, pamoja na mazingira yaliyohatarisha amani na kusababisha madhara kwa wananchi na Serikali.

Aidha, Rais Dkt. Samia amesema kuwa kazi na mapendekezo ya Tume hiyo yatakuwa ni msingi muhimu kuelekea uundwaji wa Tume ya Mazungumzo na Maridhiano, kama alivyoahidi kutekeleza ndani ya siku 100 za mwanzo za muhula wake wa pili. Akitoa msisitizo kuwa hatua hii ni sehemu ya jitihada za Serikali kujenga taifa lenye amani imara, maridhiano ya kudumu na mshikamano wa kitaifa.

Katika ufafanuzi wa kina Rais Samia amefafanua kuwa kutokana na matukio ya hivi karibuni, aliona ni muhimu kuunda Tume ya ndani mapema kabla ya kupokea timu za uchunguzi kutoka nje ya nchi, ili Watanzania wenyewe wawe wa kwanza kuchambua chanzo na hali halisi ya kilichotokea.

Katika kuelezea umuhimu wa uchunguzi huo, Dkt. Samia ameeleza kuwa ni lazima Tume ichunguze kwa makini sababu zilizowasukuma wananchi, hususan vijana, kuingia barabarani na kushiriki vurugu. Amebainisha kuwa Serikali inahitaji kujua ni haki gani ambazo vijana walihisi wamenyimwa, na ni kwa nini waliona umuhimu wa kujitokeza kwa wingi kudai haki hizo.

Ameongeza kuwa Tume inatarajiwa kuchunguza pia hatua zilizochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama wakati wa matukio hayo. Akieleza kuwa uwepo wa wastaafu wa Jeshi na Polisi katika Tume utasaidia kupata tathmini sahihi ya jinsi hatua hizo zilivyotekelezwa na maeneo yanayohitaji maboresho.

Katika hitimisho, Rais Dkt. Samia amesema kuwa Serikali tayari imetowa muongozo wa awali na itatoa rasilimali zote muhimu ili kuiwezesha Tume kufanya kazi kwa ufanisi. Kupitia taarifa na mapendekezo ya Tume, Serikali itaweza kuchukua hatua stahiki kwa ajili ya kulinda amani, haki na utulivu wa Taifa.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook