Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka wazi dira mpya ya Serikali ya Awamu ya Sita wakati akiwaapisha Mawaziri na Manaibu Mawaziri 56 jijini Dodoma, ambapo ameeleza dhamira yake ya kuharakisha maendeleo kwa kutekeleza miradi kwa kutumia rasilimali za ndani na kuimarisha uwajibikaji wa viongozi wake.

Katika hotuba yake, Rais Samia ameeleza kuwa serikali haiwezi kuendelea kutegemea wahisani kama chanzo kikuu cha kutekeleza miradi, kwa kuwa mchakato wa kupata kibali na msaada kutoka nje umekuwa ukichukua muda mrefu na kusababisha ucheleweshaji wa utekelezaji. Na sasa Serikali itaanza mkakati wa kutekeleza miradi kwa fedha zake, na hatua hiyo imelenga kuongeza kasi ya maendeleo na kuhakikisha mahitaji ya wananchi yanashughulikiwa bila kusubiri taratibu ndefu za wahisani. Katika mfumo huu mpya, mashirika ya kimataifa yataungana na serikali katikati ya ikiwa yatakubali kuungana katika utekelezaji badala ya kuwa chanzo cha kuanza mradi.
Rais Samia amesema kuwa vurugu na uharibifu uliojitokeza nchini katika siku zilizopita unaweza kupunguza uwezo wa Tanzania kupata mikopo na misaada kwa urahisi kama ilivyokuwa katika muhula wake wa kwanza. Kutokana na changamoto hiyo, amewataka Mawaziri wajipange vizuri katika utafutaji na usimamizi wa rasilimali chache zilizopo ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi unaendelea pasipo kuyumba.
Katika ujumbe wenye msisitizo mkubwa, Rais Samia pia amewakumbusha Mawaziri kuwa dhamana walizopewa sio kwa ajili ya ufahari, bali ni majukumu ya kazi yanayotakiwa kuleta matokeo kwa wananchi. Ametangaza wazi kuwa hatovumilia viongozi wanaochukulia nafasi zao kama fahari ya kutembea nayo mitaani badala ya kuwa nyenzo ya kuwahudumia wananchi. Mawaziri wametakiwa kuonyesha mfano wa uadilifu, unyenyekevu, uzalendo na kasi katika utendaji wao, huku wakifuata dira ya serikali ya Kazi na Utu.
Rais Samia ameeleza kuwa ahadi za serikali kwa wananchi ni nyingi na muda wa kuzitekeleza ni mfupi. Hivyo Mawaziri wametakiwa kubadilika, kuongeza kasi ya utekelezaji, kuimarisha ushirikiano na

kuhakikisha wananchi wanaona matokeo ya moja kwa moja katika huduma na miradi inayotekelezwa. Amesema kuwa taarifa zisizoonyesha matokeo ya kweli hazitakuwa sehemu ya utendaji serikalini, kwa kuwa wananchi wanahitaji ushahidi wa kazi na si taarifa za maneno.Mawaziri na Manaibu Mawaziri wametakiwa kuanza safari ya uwajibikaji mara moja, wakitambua kuwa miaka mitano si mingi kama haitatumika vizuri na kwa kasi inayotakiwa.
Kwa ujumla, hotuba ya Rais Samia imeweka msingi mpya wa utendaji ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita ikitoa mwanga mpya wa kuanza utekelezaji wa miradi kwa nguvu za ndani, i kwa kasi, huku ikitumia uongozi kama jukumu la kuwahudumia wananchi, si nafasi ya kujivunia.





