RAIS SAMIA AZINDUA BUNGE LA 13 AKITOA WITO WA AMANI, MAELEWANO NA MAENDELEO YA TAIFA

Scroll Down To Discover
Font size:

Dodoma, Novemba 14, 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, siku ya leo amezindua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutoa wito wa umoja, maelewano na amani nchini, huku akiongoza Wabunge pamoja na wageni waalikwa kusimama kwa heshima na kuwakumbuka wananchi waliopoteza maisha katika vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025, katika miji ya Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Songwe.

Katika hotuba yake, Rais Samia ametaja tukio hilo kama changamoto iliyohatarisha usalama wa Taifa na kusababisha uharibifu wa mali na vifo vya wananchi. Aidha Mhe Rais ametangaza kuundwa kwa Tume Maalumu ya kuchunguza matukio hayo, ikilenga kubaini chanzo cha vurugu na kutoa mwongozo wa maelewano endelevu. “Uchunguzi huu utasaidia kufahamu kiini cha tatizo na kutoa mwongozo wa namna ya kufikia maelewano na kudumisha amani nchini,” amesema Rais Samia.

Akiwa ameguswa na tukio hilo, Rais Samia alitoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu na jamaa na kuwaombea majeruhi kupona haraka. Aidha, aliwaomba wananchi waliopoteza mali zao kuwa na uvumilivu wakati Serikali ikiendelea kufanya tathmini na kuchukua hatua za kukabiliana na athari za vurugu hizo.

Rais Samia amesisitiza kuwa, licha ya uchaguzi kufanyika, matukio ya uvunjifu wa amani yameonyesha umuhimu wa Watanzania kuendelea kuongozwa na dhamira ya kuimarisha maelewano, kushirikiana na kurekebisha makosa. Akiwahimiza vijana kutoshawishiwa na kufanya vitendo vinavyohatarisha amani ya Taifa. “Ninyi ndio wajenzi, walinzi na warithi wa Taifa hili,” amesema, Mhe Rais akiwataka wananchi kushirikiana katika kuendeleza misingi ya amani na kujenga Tanzania bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha, Rais Samia amevielekeza vyombo vya sheria kufanya tathmini ya makosa yaliyofanywa na vijana waliokamatwa, na kutoa maagizo kuwa wale waliobainika kujihusisha katika vurugu kwa kufuata ushabiki bila kuelewa uzito wa matendo yao, wafutiwe mashtaka na waachiwe huru.

Katika hotuba yake, Rais pia amebainisha dhamira ya Serikali kuimarisha sekta mbalimbali za maendeleo. Akitilia mkazo wa maendeleo katika sekta ya utalii, ambapo lengo ni kuvutia watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2030. Pia alibainisha mikakati ya kuboresha miundombinu ya barabara, Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), ujenzi wa daraja la Mto Msimbazi na kuendeleza Mpango wa Gridi Imara ili kuhakikisha usambazaji thabiti wa umeme.

Rais Samia pia amesisitiza uwajibikaji na uwazi katika mashirika ya umma, kutoa haki kwa wananchi kwa wakati unaofaa, na kuahidi pia kuendelea kuimarisha Mahakama kwa kutoa vitendea kazi, watumishi waliokuwa na weledi pamoja na kuimarisha teknolojia ya TEHAMA. Aidha, ameeleza kuhusiana na mchakato wa marekebisho ya katiba kama moja ya nguzo za maelewano ya kitaifa, akibainisha kuwa jambo la kwanza itakuwa ni kuundwa kwa Tume ya Usuluhishi na Maelewano ndani ya siku 100 za muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Rais Samia pia ameweka bayana kuwa falsafa ya 4R iliyotumika katika muhula wa kwanza wa Awamu ya Sita iliunganisha Taifa katika msingi wa maridhiano na mshikamano wa kitaifa kabla ya baadhi ya wadau kutupilia mbali mkono huo wa maelewano. “Serikali inaendelea kusimamia misingi ya amani, maelewano na ustahimilivu ili kujenga nchi imara, yenye umoja na mustakabali mwema kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema.

Kwa ujumla, hotuba ya Rais Samia imeonyesha dhamira ya kuunganisha Taifa, kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiuchumi, na kutoa kipaumbele cha dhati kwa vijana na usalama wa wananchi. Aidha, ni wito wa dhati kwa Watanzania wote kushirikiana katika kujenga taifa lenye amani, utulivu na maendeleo endelevu.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook