Habari ya asubuhi. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuturuzuku uhai na kutuwezesha kushiriki sherehe hizi za kihistoria kwa Taifa letu. Pili niwashukuru Watanzania wote kwa imani yao kwa Chama cha Mapinduzi, na kwa mapenzi makubwa, na kutupa mimi na Makamu wa Rais fursa hii adhimu ya kuwatumikia.
Shukrani za kipekee kwa Viongozi na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi, kwa namna walivyoendesha kampeni kwa mafanikio makubwa.
Niishukuru tena Tume ya Uchaguzi kwa kuratibu na kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi kwa ufanisi usiotiliwa shaka.

Ndugu Viongozi; Ndugu Wananchi;
Katika Uchaguzi huu tulikuwa na wagombea 17 kutoka vyama mbalimbali vya siasa tukiwania nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda kuwashukuru wenzangu 17 ambao kwa hakika mmeonesha ukomavu wa kidemokrasia kwa kuendesha kampeni ambazo tulishindana kwa hoja, na sote tulionesha, kuwa siasa sio vita. Tumemaliza vyema uchaguzi na kumpongeza alieshinda.
Aidha, nitumie fursa hii pia kumpongeza sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi na Vyama vya Siasa vilivyokuwa kwenye mchakato wa uchaguzi, kwa kumaliza uchaguzi kwa salama na amani. Zanzibar Oyeee!
Pongezi zangu pia ziwaendee wote walioshinda kwenye nafasi za Ubunge; Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi; na Udiwani kote nchini. Kwa wote niwaambie uchaguzi umekwisha, sasa tukafanye kazi ya kulijenga Taifa letu, na Utu wa Mtanzania.
Waheshimiwa Marais; Viongozi; Ndugu Wananchi;
Shughuli inakuwa nzuri na ya kufurahisha ikihudhuriwa na wanaokupenda. Tanzania leo imejawa na furaha kubwa kuona baadhi ya Waheshimiwa Marais wenzangu na viongozi mbalimbali wa nchi jirani wamejumuika nasi katika tukio hili, pamoja na kwamba tulitoa mwaliko kwa muda mfupi. Kwa wale walioshindwa kushiriki tunatambua uzito wa majukumu yao, na tunajua mioyo yao ipo pamoja nasi. Tunawashukuru pia wote waliotuma salamu za pongezi kwetu. Tunasema ahsanteni sana.
Ndugu Wananchi;
Uchaguzi ni fursa kwa Wananchi kueleza matakwa yao ya aina ya viongozi wanaodhani wataweza kuwatumikia vyema, na kuwaletea maendeleo endelevu. Kipindi cha kampeni tuligawika kiitikadi na kishabiki kama taifa. Ila baada ya uchaguzi kufanyika, anaechaguliwa na wengi huwa ndio chaguo la nchi na anapaswa kuwa Mtumishi wa Wananchi wote, waliomchagua, waliochagua wagombea wengine, na hata ambao hawakushiriki uchaguzi. Kwa sisi tuliochaguliwa, ahadi yetu ni kulitumikia Taifa hili kwa nguvu zetu zote, vipawa vyetu vyote na maarifa yetu yote.
Ndugu zangu Watanzania, ni vyema tutambue kuwa uchaguzi mkuu wa Viongozi wa Serikali ni mchakato wa msimu mmoja tu ndani ya miaka mitano. Muda mwengine wote maisha lazima yaendelee. Hivyo basi, Jukumu letu sote kwa pamoja, ni kujenga nchi yetu na kuifanya kesho yetu iwe bora zaidi kuliko jana yetu. Niwasihi tuendelee kuilinda itikadi yetu ya umoja na mshikamano.
Ndugu Wananchi;
Wote tunaoitakia mema nchi hii tumesikitishwa na kuhuzunishwa na matukio ya uvunjifu wa amani, upotevu wa maisha na uharibifu wa mali za Umma na mali za Watu binafsi kwenye baadhi ya maeneo nchini, hasa kwenye Majiji na Miji. Kilichotokea hakiendani na taswira na sifa za Kitanzania na sio Utanzania. Haikutushangaza kuona kuwa baadhi wa vijana waliokamatwa kutokana na kadhia hio wametoka nje ya Tanzania. Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vinaendelea kufuatilia na kuchunguza kwa undani zaidi kilichotokea, na kuirudisha nchi katika hali tuliyoizowea kwa haraka. Kamati ya Ulinzi ya Kitaifa, na Kamati za Ulinzi za Mikoa na Wilaya, hakikisheni kuanzia leo maisha ya Wananchi yanarejea mara moja. Pia nitumie fursa hii, kutoa onyo kwa wale wote waliochochea uvunjifu wa amani, na nawataka watambue kuwa vurugu na uvunjifu wa amani huishia kupimana nguvu na uwezo wa kujihami, ila mazungumzo huzaa mshikamano. Tuchague lenye manufaa kwetu, kwani usalama wa Taifa lolote hulindwa na wote kwa nguvu na gharama zozote.
Ndugu Viongozi; Ndugu Wananchi;
Kama kawaida, kwa nchi zenye mfumo wa Kidemokrasia hualika waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya za Kimataifa na Kikanda kuja kushuhudia mchakato wa uchaguzi. Uwepo wao huongeza uhalali wa juhudi zetu za kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwenye mazingira ya uwazi, haki, heshima na utawala wa sheria. Kwa muktadha huu, tunazishukuru Jumuiya zote zilizoleta waangalizi wa uchaguzi. Kutoka Afrika tulikuwa na waangalizi kutoka Umoja wa Afrika (AU); Jumuiya ya nchi za Maziwa Makuu (ICGLR); Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika (SADC); na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Pamoja na hao, tulikuwa na wengine kutoka maeneo mbalimbali. Makundi yote ya waangalizi yameshatoa taarifa za awali, na tunawashukuru kwa kuwa nasi, na kwa heshima kubwa tumepokea maoni yenu. Hata hivyo, kama alivyowahi kusema Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa mwaka 2000 wakati akiapishwa kuwa Rais, na hapa ninakinukuu kipande cha Hotuba hiyo, kinachosema
‘’nawashukuru watazamaji wa kimataifa kuja kushuhudia uchaguzi wetu ulivyofanyika, walipotusifia tumepokea sifa hizo kwa unyenyekevu. Tumesikia pia waliyodhani hayakwenda sawa na mengine hata sisi tumeyaona. Maagizo yao tumeyakataa, ushauri wao tutauzingatia ili tufanye vizuri zaidi siku zijazo.”
Ndugu Wananchi;
Sifa moja ya Mwanadamu ni kutokukamilika, aliekamilika kabisa kabisa bila kasoro yoyote ni Mwenyezi Mungu peke yake. Ndio maana, katika shughuli au harakati za wanaadamu tunaunganishwa na mawasiliano, mazungumzo na maelewano, au kwa maneno mengine, tunaunganishwa na uwepo wa Suluhu ya mambo katika jamii zetu. Kama mnavyofahamu, katika kuliunganisha Taifa, Serikali ya awamu ya sita tulianza na falsafa ya 4R’s, inayosimamia misingi ya kuzungumza na kuelewana (Reconciliation), kuvumiliana (Resilience), kubadilisha mwelekeo baada ya maelewano (Reforms) na kuendelea kujenga Taifa letu (Re Construction/Building). Tunapoendelea mbele hatutachoka wala kurudi nyuma kwenye kusimamia yote yanayohusu kujenga Umoja na Mshikamano wa Taifa letu.
Ndungu Watanzania;
Mkusanyiko wetu leo hapa, sio kwa ajili ya kuzawadia walioshinda kwenye uchaguzi, la hasha; bali ni matakwa ya kikatiba ya kukabidhiwa dhamana ya kuwa mtumishi mkuu wa Taifa katika kuleta maendeleo endelevu; kwa maana ya uimara wa Kiuchumi, Kisiasa, kidiplomasia na Kijamii. Ili tuweze kuyatimiza hayo, hatuna budi kuhakikisha tunahimizana umoja na upendo kwa nchi yetu, tunadumisha amani na kuheshimu sheria za nchi. Kinyume cha hayo, Maandamano, vurugu na uvunjifu wa amani, husababisha maumivu na havileti manufaa wala faida kwa yeyote.

Niwasihi Watanzania tuchague hekima badala ya ghadhabu; busara badala ya mihemuko; upendo badala ya chuki; uvumilivu badala ya vinyongo; umoja badala ya mgawanyiko; amani badala ya vurugu; unyenyekevu badala la kiburi; na huruma badala ya hasira. Taifa letu ni bora na lina nguvu zaidi kuliko mtu yeyote. Demokrasia haipimwi kwa nani kashinda uchaguzi, bali kwa jinsi tunavyoendesha mambo yetu baada ya uchaguzi. Tutakuwa na nguvu zaidi pale kila sauti, chanya na hasi, zinaposikilizwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa, na vile vile, tunapoweza kuponya penye maumivu. Hii si kazi ya upande mmoja wa Serikali peke yake, bali ni kwa kila Jumuiya za Wananchi, Chama cha Siasa, Dini zetu, na kila mwananchi. Na hapa, nitumie fursa hii, kuwashukuru kwa dhati ya moyo wangu Viongozi wa Dini waliohimiza amani na upendo katika kipindi chote cha uchaguzi.
Ndugu Wananchi;
Nimeamua kutumia jukwaa hili leo kushukuru na kupongeza kwa kumaliza uchaguzi, kuhimiza Umoja na Mshikamano wa Kitaifa na kusisitiza kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Taifa ni muhimu zaidi kuliko matakwa binafsi ya mtu yeyote. Masuala ya mwelekeo wa kazi za Serikali kwa miaka mitano ijayo, na ufafanuzi wa kina wa hatua zitakazochukuliwa kutekeleza dhana ya Kazi na Utu utatolewa katika hotuba ya uzinduzi wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya kusema hayo, niwashukuru wote kwa kujumuika nasi kwenye tukio hili muhimu na la kihistoria. Nimepokea pongezi zote kwa heshima kubwa, na sasa safari ya kuwatumikia Watanzania kwa kipindi cha pili inaanza rasmi.





