Mgombea wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameeleza kuwa ajenda kuu tatu za chama hicho katika kuongoza taifa ni kuliheshimisha taifa la Tanzania ndani na nje ya nchi, kukuza maendeleo ya kiuchumi, na kuboresha huduma za kijamii kwa Watanzania wote.
Akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Mnadani, Sengerema, Dkt. Samia alisema serikali itaendelea kuwekeza katika kilimo, uvuvi na ufugaji kwa kuhakikisha mazao na bidhaa za mifugo zinapata soko, huku wakulima na wafugaji wakinufaika kupitia ruzuku za pembejeo na chanjo za mifugo.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kujenga maghala na vihenge vya kisasa kwa ajili ya kutunza mazao ya chakula na biashara, akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza thamani ya mazao na kudhibiti upotevu unaotokea baada ya mavuno.
Dkt. Samia alisema serikali imeendelea kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima na kuhakikisha mifugo kama ng’ombe, mbuzi na kondoo inachanwa kwa bei nafuu au bure, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha sekta ya kilimo na mifugo nchini.
Katika kuimarisha uchumi wa wananchi, Dkt. Samia alieleza kuwa serikali ina mpango wa kujenga viwanda katika kila wilaya ili kuongeza ajira na kuongeza thamani ya bidhaa za ndani, sambamba na kuanzisha vizimba 400 vya kufugia samaki kwa lengo la kukuza sekta ya uvuvi.
Aidha, alisisitiza kwamba kuliheshimisha taifa ni wajibu wa kila Mtanzania, akieleza kuwa amani na utulivu uliopo umeifanya Tanzania kuheshimika kimataifa. Aliongeza kuwa Watanzania wanapaswa kuendelea kudumisha umoja na utulivu, kwani ni msingi wa maendeleo ya taifa.
Dkt. Samia alitumia nafasi hiyo kuahidi kuendeleza juhudi za kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya, maji safi, elimu bila ubaguzi, na nishati ya uhakika, huku serikali ikiendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kijamii na kiuchumi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Dkt Samia ameeleza kuwa, utekelezaji wa ajenda hizo tatu utaendelea kuimarisha uchumi wa taifa, kuongeza ustawi wa wananchi, na kulinda hadhi ya Tanzania katika jamii ya kimataifa.





