RAIS DK. SAMIA SULUHU HASSAN ATAJA NEEMA MPYA KWA WANA TABORA

Scroll Down To Discover
Font size:

Mgombea wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea na ziara yake ya kampeni mkoani Tabora, ambako ameahidi miradi mikubwa ya maendeleo inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.

Katika sekta ya kilimo, Dkt. Samia ameweka msisitizo mkubwa kwenye zao la tumbaku, akiwahakikishia wakulima kuwa madeni yao yamelengwa kulipwa kupitia mazungumzo yanayoendelea na kampuni zinazodaiwa. Ameeleza kuwa serikali yake imeongeza ushindani kwa kuhamasisha kampuni nyingi zaidi kununua tumbaku, jambo lililopelekea kupanda kwa bei na kuongeza mapato ya wakulima.

Aidha, Dkt. Samia ameahidi kuimarisha sekta ya mifugo kwa kuanzisha ranchi za kisasa, minada, machinjio na majosho ili kusaidia wafugaji kupata mifugo bora yenye ushindani katika soko la kimataifa.

Sekta ya elimu pia imepewa kipaumbele, ambapo amesisitiza kuwa serikali imeongeza shule za msingi na sekondari, imejenga vyuo vya ufundi, na itaendelea kuongeza miundombinu kadri mahitaji yanavyoongezeka. Vilevile, ameahidi kuajiri walimu wapya 7,000 nchi nzima ili kuimarisha ubora wa elimu.

Katika afya, Dkt. Samia amesema serikali imetenga fedha kwa ajili ya kujenga na kuboresha vituo vya afya, hospitali na zahanati. Amesisitiza kuwa ndani ya siku 100 za awali za serikali atakayoongoza, watumishi 5,000 wa afya wataajiriwa, ili kuimarisha huduma katika maeneo ya vijijini na mijini.

Kwenye sekta ya maji, ameweka wazi kuwa miradi mikubwa kama ule wa maji ya Ziwa Victoria imekamilishwa, na pia kuwakumbusha kuwa serikali inaendelea na uchimbaji visima pamoja na miradi ya maji vijijini kuhakikisha kila kaya inapata huduma ya maji safi na salama.

Dkt. Samia pia ameahidi ujenzi wa barabara za kiwango cha lami zinazounganisha wilaya mbalimbali za Tabora na mikoa jirani, pamoja na kujenga soko la kisasa, stendi kuu ya mabasi, na miundombinu ya kuongeza thamani ya mazao ya wakulima.

Akiwa Uyui, Dkt. Samia amewahakikishia wakulima kuwa malipo yao hayatacheleweshwa tena, na kwamba serikali imejipanga kuondoa changamoto za muda mrefu zinazokwamisha sekta ya kilimo.

Katika hotuba zake, Dkt. Samia ameendelea kuhimiza mshikamano, mshikikano wa chama na wananchi, huku akisisitiza kuwa ushindi wa CCM ni fursa ya kuendeleza kasi ya maendeleo kwa Tabora na taifa kwa ujumla.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook