RAIS DK. SAMIA AZINDUA BANDARI KAVU YA KWALA NA SAFARI ZA MIZIGO ZA SGR

Scroll Down To Discover
Font size:

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameandika historia mpya ya mageuzi ya kiuchumi kupitia sekta ya usafirishaji, hii ni baada ya kuzindua rasmi Bandari Kavu ya Kwala iliyopo Mkoani Pwani, pamoja na kuzindua rasmi kwa safari za mizigo kwa kutumia Reli ya Kisasa (SGR), ifikapo Agosti 4, 2025. Uzinduzi huu ni hatua ya kimkakati inayolenga kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, kupunguza gharama za usafirishaji, kurahisisha shughuli za uchukuzi, na kuongeza ufanisi wa bandari na biashara kwa ujumla.

Katika hotuba yake, Mhe. Rais Samia ameelza kuwa maendeleo haya makubwa ni sehemu ya maandalizi ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji na biashara kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, sambamba na ushiriki wa nchi katika Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA). Aidha, amebainisha kuwa safari za mizigo kwa kutumia SGR kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Kwala zitatumia dakika 45 hadi saa moja, na safari za kwenda Dodoma zitachukua masaa manne hadi matano, ikilinganishwa na wastani wa masaa 30 hadi 35 kwa malori. Hatua hii ni sehemu ya jitihada za kupunguza uchakavu wa barabara, kuimarisha ulinzi wa mazingira, na kuongeza ushindani wa kiuchumi kwa nchi yetu.

Rais Samia pia, ameeleza kuwa serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 330 katika ununuzi wa mabehewa 1,430 ya mizigo kwa ajili ya SGR, huku kampuni kama GSM na Bakhresa tayari zikiwa zimeanza kutumia reli hiyo. Mhe Rais amelitaka shirika la reli nchini TRC na Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha mabehewa hayo yanatumika ipasavyo kwa kuweka watu wenye weledi na ubunifu katika vitengo vya biashara na mauzo, huku sekta binafsi ikiombwa kushiriki kwa kununua vichwa vya treni na mabehewa yao, na kushirikiana na serikali kwa utaratibu maalum.

Katika hotuba yake pia ameeleza kuwa Bandari Kavu ya Kwala imejengwa kwa viwango vya kisasa na tayari imeanza kuvutia wawekezaji wa ndani na nje walioko tayari kuwekeza katika viwanda na biashara. Mhe Rais amebainisha kuwa Kongani ya Kwala inatarajiwa kuwa na viwanda 200 na kutoa ajira 50,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja 150,000, jambo linaloonesha dhamira ya serikali ya kuijenga Tanzania ya viwanda kwa vitendo. Kituo hicho pia kitatoa huduma bora kwa wafanyabiashara wa ndani na wale wa nchi jirani kama DRC, Burundi, Zambia, Rwanda na Malawi, kwa kuwa mizigo itaweza kuhifadhiwa, kuchakatwa na kusambazwa kutoka Kwala bila kulazimika kwenda bandarini Dar es Salaam.

Rais Samia amesisitiza kuwa serikali inalenga kuhakikisha kuwa mteja wa bandari anaweza kuagiza mzigo kutoka popote duniani na kuchukulia Kwala, kwa kutumia CIF ya Kwala badala ya Dar es Salaam. Pia alieleza kuwa serikali imeanza hatua za usanifu wa ujenzi wa ghati kubwa ya kisasa Mbegani – Bagamoyo yenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa zenye uwezo wa kubeba makasha 24,000 sawa na tani 600,000 kwa wakati mmoja, hatua ambayo itaiwezesha Tanzania kuongeza ushindani wa bandari zake na kurahisisha biashara kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook