RAIS SAMIA AZINDUA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050.

Scroll Down To Discover
Font size:

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameandika ukurasa mpya katika historia ya maendeleo ya taifa kwa kuzindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuijenga Tanzania yenye uchumi imara, jamii jumuishi na ustawi kwa wote. Uzinduzi huo umefanyika jijini Dodoma, ambapo Rais Samia amebainisha kuwa utekelezaji wa dira hiyo utaanza rasmi Julai 1, 2026, mara baada ya kukamilika kwa Dira ya Maendeleo 2025.

Katika hotuba yake, Rais Samia amesema kuwa Dira ya 2050 inalenga kuwa dira ya kizazi kijacho kwa kulenga sekta muhimu kama kilimo, viwanda, madini, utalii, uchumi wa buluu, michezo, ubunifu na huduma za kijamii, ambazo zitachochea ukuaji wa sekta nyingine na kuongeza thamani ya uzalishaji wa taifa. Amesema thamani halisi ya dira hiyo itapimwa kupitia utekelezaji wa sera, bajeti na maamuzi ya kila siku ya serikali, sekta binafsi na jamii kwa ujumla. Huku akisisitiza kuwa huu si wakati wa kusema bali ni wakati wa kutenda.

Katika uzinduzi huo, Rais Samia ametoa maagizo mahsusi kwa wizara zote nchini kupitia upya sera zao na kuhakikisha zinaendana na maudhui ya Dira ya 2050, huku akiiagiza Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya uchambuzi wa sheria zinazohitaji maboresho ili kuwezesha utekelezaji wake. Pia amehiimiza uwepo wa viashiria vya kupima mafanikio kwa kila taasisi na kutaka taarifa za utekelezaji ziwe wazi na kupatikana kwa umma.

Katika kuelekea malengo makuu ya kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu, yenye pato la taifa la zaidi ya Dola trilioni moja na pato la mtu mmoja la Dola 7,000 kwa mwaka, Rais Samia amesisitiza haja ya mabadiliko ya fikra, mitazamo na vitendo. Akibainisha kuwa hakuna nafasi ya kufanya kazi kwa mazoea na kusisitiza umuhimu wa uwajibikaji wa pamoja katika utekelezaji wa dira hii. Rais Samia amemtaja Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, kuwa msimamizi mkuu wa utekelezaji wa Dira ya 2050, akibeba jukumu kubwa la kuhakikisha dira hii inatekelezeka.

Pia, Rais Samia ameeleza kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya ukuaji wa uchumi, hivyo serikali itaweka mazingira rafiki kwa maendeleo ya sekta hiyo, huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa dira hii unahitaji ushirikiano wa karibu baina ya serikali, sekta binafsi na jamii nzima. Rais katika hotuba yake ameagiza kuandaliwa kwa mkakati wa mawasiliano, elimu kwa umma na uhamasishaji kuhusu Dira ya 2050 ili kuhakikisha kila Mtanzania anaifahamu na anashiriki katika ujenzi wa taifa.

Aidha, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa Tanzania kushiriki kikamilifu katika masuala ya kimataifa kwa kulinda maslahi ya taifa katika mazingira mapya ya dunia. Amesema kuwa Tanzania itaendelea kuwa nchi isiyofungamana na upande wowote, lakini yenye msimamo thabiti katika diplomasia ya kimataifa, maendeleo ya kijamii, utunzaji wa mazingira na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Mhe Rais ametoa wito kwa taifa kutumia teknolojia kwa manufaa ya maendeleo, huku tukilinda ajira na ustawi wa watu wote.

Rais Samia amesisitiza pia umuhimu wa taasisi za kisheria na haki za binadamu kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa dira hii kwa kuhakikisha usawa, haki, uwajibikaji na utawala bora. Amesema kuwa Tanzania ya miaka 25 ijayo lazima ijengwe juu ya msingi wa haki, maadili na utamaduni wa uwajibikaji wa kitaifa.

Katika muktadha huo, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imejengwa juu ya misingi sita ikiwemo maendeleo jumuishi, uchumi shindani, usawa wa kijinsia, uendelevu wa mazingira, ustawi wa jamii na ukuaji wa kipato cha mtu mmoja mmoja. Malengo makuu ya dira hii ni pamoja na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu, kutokomeza umasikini uliokithiri, na kuifanya kuwa mzalishaji mkuu wa chakula barani Afrika na miongoni mwa nchi 10 bora duniani kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Katika maandalizi ya dira hii, zaidi ya watu milioni 1.1 walishiriki kutoa maoni, wengi wao wakiwa vijana kati ya umri wa miaka 15 hadi 35. Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, asilimia 81 ya waliochangia maoni kwa njia za kidijitali walikuwa vijana, ishara ya nguvu ya kizazi kipya katika kupanga hatma ya taifa lao. Rais Samia amesisitiza kuwa dira hii ni ya vijana, na ni lazima vijana waweke mikakati ya kuitekeleza kwa vitendo, kwani wao ndio watakaokuwa mashahidi wa mafanikio au kushindwa kwake.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook