Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, amewaagiza Wakuu wa Mikoa kote nchini kusimamia ipasavyo sekta ya kilimo kwa kuhakikisha inakuwa kipaumbele katika maeneo yao, ikiwa ni hatua ya kuimarisha uzalishaji na mchango wa kilimo katika uchumi wa taifa.
Mhe. Rais Samia alitoa maagizo hayo jana, wakati wa uzinduzi wa Kiwanda cha Mbolea cha Itracom kilichopo Tanzania, ambacho kimejengwa kwa uwekezaji wa takribani Shilingi bilioni 480.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji kuhakikisha uzalishaji wa mbolea unaongezeka, hususan mbolea zenye ubora na zinazozingatia mahitaji ya afya ya udongo kwa manufaa ya wakulima.

"Ni muhimu menejimenti ya kiwanda hiki kushirikiana na watafiti wetu wa ndani ili kuimarisha elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea. Hii itasaidia kuongeza tija katika kilimo, mapato ya wakulima na hatimaye kuchochea maendeleo ya taifa letu," alisema Mhe. Rais Samia.
Aidha, ameitaka menejimenti ya Itracom kuhakikisha mfumo wa usambazaji wa mbolea unafika hadi vijijini kwa bei nafuu, ili kuwezesha wakulima wengi zaidi kunufaika na uwekezaji huo.
Kwa upande wa Watanzania waliopata ajira kupitia kiwanda hicho, Rais Samia amewataka kufanya kazi kwa bidii na uaminifu ili kuchochea mazingira bora ya uwekezaji na kufanikisha malengo ya kiwanda hicho.
"Mwekezaji ameonesha imani na Tanzania kwa kuwekeza hapa, nasi tumuoneshe imani hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu," alisisitiza.
Kwa upande wake, Rais wa Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye, aliyeshiriki hafla hiyo, alisema uzinduzi wa kiwanda hicho ni kielelezo cha ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Burundi, hasa katika nyanja za kilimo na biashara.
"Kupatikana kwa mbolea bora na kwa bei nafuu kutachochea uzalishaji wa mazao, kuongeza usalama wa chakula na mapato ya wakulima katika nchi zetu. Vilevile, uwepo wa kiwanda hiki ni fursa kubwa ya kuvutia wawekezaji zaidi kuja Tanzania," alisema Rais Ndayishimiye.
Aidha, alitoa wito kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji nchini Burundi, akieleza kuwa ushirikiano wa muda mrefu wa mataifa hayo mawili unazidi kuimarika, huku akitolea mfano mabadiliko kutoka Warundi waliokuwa wakija Tanzania kama wakimbizi, hadi sasa wanakuja kama wawekezaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Itracom, Bw. John Chiligati, aliahidi kuwa kiwanda hicho kitalenga kuzalisha mbolea bora na nafuu, itakayowafikia wakulima kwa wakati na kuwawezesha kuongeza tija, kukuza kipato na kupambana na umaskini vijijini.





