Katika kilele cha kufunga pazia la Bunge la 12, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa hotuba ya kihistoria iliyochukua takribani saa mbili na nusu, akitoa mwelekeo wa taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu pamoja na taarifa ya utekelezaji wa ahadi na miradi ya maendeleo kwa miaka minne toka alipoingia madarakani.
Akihutubia bunge hilo jana jioni jijini Dodoma, Rais Dk. Samia alitangaza rasmi kufungwa kwa shughuli za Bunge hilo, ambalo litavunjwa rasmi ifikapo Agosti 3, mwaka huu, na kufungua ukurasa wa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwezi Oktoba 2025.
UCHAGUZI HURU NA WA HAKI
Katika hotuba yake, Rais Dk. Samia amesisitiza dhamira ya serikali ni kuhakikisha uchaguzi utakaofanyika mwaka huu unakuwa huru, haki na wenye kufuata sheria, akitoa mwito kwa vyama vya siasa kutoa fursa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Aidha, Mhe Rais amewasihi wagombea kuepuka lugha chafu, matusi, vurugu na vitendo visivyostahili, akisisitiza kuwa uchaguzi ni nyenzo ya kuimarisha amani, utulivu na demokrasia nchini.
“Kama nilivyosema, tubishane kwa hoja na tushindane kwa ilani zetu, kamwe tusiruhusu uchaguzi uwe chanzo cha kuvuruga amani bali tuhakikishe inakuwa nyenzo ya kuimarisha amani na utulivu wa taifa letu,” alisisitiza Rais Dk. Samia.
TUME HURU YA UCHAGUZI NA DEMOKRASIA
Akiwa Bungeni, Rais Dk. Samia ametangaza mafanikio makubwa katika kuimarisha misingi ya demokrasia nchini, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa mara ya kwanza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa sheria maalum, kufutwa kwa utaratibu wa mgombea kupita bila kupingwa, na utoaji wa ruzuku ya shilingi bilioni 87 kwa vyama vya siasa vinavyostahili.
Pia, ametangaza kukamilika kwa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura nchi nzima na kwamba INEC itatangaza tarehe rasmi ya uchaguzi na idadi ya wapiga kura katika kipindi kifupi kijacho.

MAENDELEO NA MAFANIKIO YA SERIKALI
Katika sekta ya kilimo, Rais Dk. Samia ametangaza mafanikio mengi, ikiwemo ya ongezeko la ruzuku ya mbolea hadi kufikia shilingi bilioni 300, hatua iliyochochea uzalishaji wa mazao kwa asilimia 33 na kuiwezesha nchi kuwa na utoshelevu wa chakula kwa asilimia 128.
Aidha, amebainisha kuwa serikali imeongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 561,383 mwaka 2021 hadi hekta 983,426 mwaka jana kupitia miradi 780 ya umwagiliaji, huku malengo yakiwa kufikia zaidi ya hekta milioni moja kwa kutumia maji ya Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.
MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA
Katika kipindi cha miaka minne, serikali imefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi, uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya, ambapo kilo milioni 4.9 za dawa hizo zimekamatwa na watuhumiwa zaidi ya 25,000 kukamatwa.
Pia, vituo vya tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya vimeongezeka kutoka tisa mwaka 2020 hadi 18 mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya kulinda afya za Watanzania, hususan vijana walioathirika na matumizi ya dawa hizi.

KUIMARISHA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA
Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kazi ya vyombo vya ulinzi na usalama kwa kujenga vituo 472 vya polisi hadi ngazi ya kata na shehia, kuboresha makazi ya askari na kununua magari na pikipiki za kisasa kwa ajili ya shughuli za kiutawala na operesheni.
Rais Dk. Samia pia amelitaka Jeshi la Polisi kuongeza jitihada katika kukomesha vitendo vya utekaji na watu kupotea, akieleza kuwa uhalifu mwingi unazuiwa kwa nguvu kubwa kuliko unaoonekana hadharani.
DENI LA TAIFA NA MAELEZO YA UFAFANUZI
Akizungumzia deni la taifa, Rais Dk. Samia alifafanua kuwa ongezeko lake linatokana na mikopo mipya na mikopo iliyosainiwa katika awamu zilizopita, ambayo fedha zake zimepokelewa katika kipindi cha awamu ya sita.
Aidha, mabadiliko ya thamani ya dola ya Marekani dhidi ya Shilingi ya Kitanzania yamechangia pia kuonekana kwa ongezeko la deni hilo linapokokotolewa kwa fedha za ndani.
MCHAKATO WA KATIBA MPYA NA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI
Rais Dk. Samia ametangaza kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya utaanza rasmi katika kipindi kijacho cha miaka mitano, kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030.
Pia, amebainisha kuwa uhuru wa vyombo vya habari nchini umeimarika, ambapo hadi sasa serikali imetoa leseni kwa magazeti na majarida 356, vituo vya redio 247, televisheni 68, redio na televisheni za mtandaoni 325 pamoja na blogs 72.
Rais Dk. Samia amesema serikali haijawahi kufanya uhakiki wa habari kabla ya kuchapishwa, badala yake imejikita katika kuamini weledi wa waandishi na uhuru wa habari kama nguzo ya demokrasia na maendeleo ya taifa.
MUUNGANO NA UMOJA WA TAIFA
Kwa upande wa Muungano, Rais Dk. Samia amesema bado unaendelea kuimarika, ambapo hoja 15 za Muungano zimetafutiwa ufumbuzi ndani ya miaka minne iliyopita, hatua inayojenga imani na mshikamano wa kitaifa.
Pia, amepongeza ushirikiano uliopo miongoni mwa Watanzania licha ya tofauti za kisiasa, kidini, mila na desturi, akieleza kuwa taifa linaendelea kuwa imara na lenye mshikamano mkubwa.
HITIMISHO
Katika kuhitimisha, kwa mara nyingine, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amewasihi Watanzania wote kushiriki uchaguzi mkuu kwa amani, utulivu, na kufuata sheria, huku vyama vya siasa vikihimizwa kushindana kwa sera na ilani na si kwa lugha za matusi na vurugu.
“Tanzania ni yetu sote, tuendelee kuilinda, kuijenga na kuimarisha demokrasia yetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo,” amesisitiza Rais Dk. Samia.





