MRADI WA MAJI WA SHILINGI BILIONI 12.8 WAZINDULIWA LAMADI – SIMIYU

Scroll Down To Discover
Font size:

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi mradi mkubwa wa maji katika kata ya Lamadi, Wilaya ya Busega, mkoani Simiyu. Mradi huo umegharimu shilingi bilioni 12.8 na unalenga kuhudumia zaidi ya wananchi 85,000 kutoka vijiji vya Lamadi, Lutubiga na Mkula.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, mradi huu una chanzo chenye uwezo wa kuzalisha hadi lita milioni 4 za maji kwa siku.

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, ameeleza kuwa kabla ya utekelezaji wa mradi huu, wananchi wa Lamadi walikuwa wakipata huduma ya maji kwa asilimia 23 pekee. Baada ya kukamilika kwa mradi, upatikanaji wa maji umefikia asilimia 97, hatua ambayo imetatua kwa kiwango kikubwa changamoto ya maji safi na salama katika eneo hilo.

“Rais Samia umebeba ajenda ya maji kwa vitendo. Uwepo wa mradi huu umethibitisha dhamira yako ya dhati ya kumtua mama ndoo kichwani,” amesema Mhe. Aweso.

Akizungumza mara baada ya kuzindua mradi huo, Mhe. Rais Samia ameipongeza Wizara ya Maji kwa kusimamia kwa mafanikio utekelezaji wa mradi huo na kuwataka wananchi wa Lamadi kutumia fursa hiyo kwa kuongeza uzalishaji na kuimarisha maisha yao.

“Tunaendelea kuhakikisha huduma bora za kijamii kama maji, afya na elimu zinapatikana kwa wananchi wote. Serikali imeweka mazingira bora, sasa ni wakati wa wananchi kuongeza juhudi katika kazi, kilimo na uzalishaji ili kukuza uchumi wa familia na taifa,” amesema Mhe. Rais.

Aidha, Mhe Rais amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu ili kuwezesha serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa ustawi wa wananchi.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook