RAIS SAMIA AZINDUA DARAJA LA J.P. MAGUFULI – KIGONGO–BUSISI

Scroll Down To Discover
Font size:

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Daraja la J.P. Magufuli (Kigongo–Busisi) ambalo ni sehemu ya miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3.0 na barabara unganishi ya kilomita 1.66 limekamilika kwa asilimia 100, likiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia aliyourithi mradi huo ukiwa kwenye hatua ya asilimia 25 kutoka kwa mtangulizi wake, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Mradi huo umegharimu shilingi bilioni 700 zilizotolewa na Serikali na kusimamiwa na TANROADS. Ujenzi wa daraja hilo umehusisha kampuni kutoka China, ukiwa umetoa ajira zaidi ya 29,000 tangu ulipoanza Februari 2020, ambapo asilimia 93 ya ajira zote zilitolewa kwa wazawa. Daraja hilo linaunganisha barabara kuu ya Usagara–Sengerema–Geita na ni kiunganishi muhimu kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na nchi jirani.

Rais Samia amebainisha kuwa kukamilika kwa daraja hilo ni heshima kwa Taifa na hatua kubwa ya kihistoria katika kuboresha huduma za usafiri na uchumi wa wananchi wa Kanda ya Ziwa. Mhe Rias amesema kuwa Serikali imekuwa ikiboresha miundombinu ya usafiri kwa hatua kwa hatua tangu mwaka 1968 ilipoanza kununua vivuko vya kuvusha abiria katika eneo hilo, na sasa historia hiyo imefikia hatua ya juu zaidi kwa kuwa na daraja la kudumu.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Paschal Ambrose, ameeleza kuwa daraja hilo limejengwa kwa teknolojia ya madaraja marefu likiwa na nguzo kuu tatu zenye kimo cha mita 40, pamoja na nguzo nyingine 64 zilizopangwa kwa umbali tofauti kulingana na usanifu. Pia kuna njia mbili za magari, njia ya dharura, na njia za watembea kwa miguu kila upande, yote ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha usalama na ufanisi wa usafiri wa barabara kati ya Kigongo na Busisi.

Baada ya uzinduzi huo wananchi mkoani Mwanza na Geita wameeleza furaha yao kwa kukamilika kwa mradi huo, wakielezea kuwa daraja hilo litarahisisha shughuli za uchumi, biashara na usafiri kwa ujumla. Wnanchi hao wameeleza kuwa muda wa safari umepungua kwa kiasi kikubwa, na sasa wataweza kusafirisha bidhaa kwa haraka na kwa uhakika, hali inayoongeza tija na kipato.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook