Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imeamua kuipa msukumo mkubwa elimu ya amali na ufundi ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri au kuajiriwa moja kwa moja baada ya kuhitimu sekondari.
Akizungumza katika Wilaya ya Itilima, mkoani Simiyu, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mwamapalala Amali, Rais Samia amesema mwelekeo wa sasa wa elimu ni kuhakikisha kila mwanafunzi anapomaliza sekondari, anakuwa na stadi na ujuzi wa moja kwa moja unaomwezesha kuingia sokoni.
Rais Samia amesema hatua hiyo ni sehemu ya mageuzi makubwa yanayofanywa na Serikali katika sekta ya elimu, ikijumuisha ujenzi wa shule mpya 26 za amali na ufundi zinazoendelea kote nchini kwa gharama ya shilingi bilioni 41.6. Amesisitiza kuwa ifikapo Januari 2026, shule hizo zitapokea wanafunzi, hivyo ni wajibu wa wazazi kuhakikisha vijana wao wanatumia fursa hizo kwa maendeleo yao binafsi na ya Taifa.
Aidha, Rais Samia pia amewataka wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa shule hizo kuhakikisha wanakamilisha kazi kwa wakati ili wanafunzi waanze masomo kama ilivyopangwa. Ameeleza kuwa Serikali inawekeza fedha nyingi kuboresha elimu, kutoka shule za msingi hadi vyuo vikuu, hivyo wananchi wanapaswa kuzitumia fursa hizo kikamilifu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, akizungumza amebainisha kuwa shule hizo ni sehemu ya mpango wa kuimarisha elimu ya kati kwa kujenga uwezo wa wahitimu kupitia vyeti, diploma, hadi elimu ya juu. Naye Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, amesema shule ya Mwamapalala pekee inagharimu shilingi bilioni 1.6 katika ujenzi wake
Katika hatua nyingine, akiwa wilayani Bariadi, Rais Samia amemuagiza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kuanzisha na kusimamia ushirika wa pamba mkoani Simiyu ili kuimarisha thamani ya zao hilo. Amesisitiza kuwa ushirika bora utasaidia kupandisha hadhi ya pamba, kuongeza faida kwa wakulima, na kuchochea uchumi wa ndani kwa kuhakikisha pamba inachakatwa nchini badala ya kusafirishwa ghafi kwenda nje.
Rais Samia ametoa pia maelekezo ya kuanzishwa kwa Ofisi ya Tume ya Umwagiliaji katika mikoa ya Simiyu na Dodoma ili kusogeza huduma karibu na wakulima, pamoja na kuharakisha kukamilika kwa miradi ya barabara na madaraja kama Daraja la Itende, barabara za ndani za TARURA na miundombinu mingine muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa Simiyu.
Kwa ujumla, ziara ya Rais Samia mkoani Simiyu imeonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, kukuza uchumi wa ndani na kujenga jamii yenye ujuzi, ustawi na maendeleo endelevu.






