Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 9 Juni 2025, ameshiriki sherehe ya kufunga kozi ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi katika viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Polisi, Kurasini, Jijini Dar es Salaam.
Akihutubia kwenye hafla hiyo, Mhe. Rais amelipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua kubwa linazopiga katika maboresho ya ndani, akisisitiza kuwa tayari mabadiliko makubwa yameanza kuonekana. “Hata ukiangalia nidhamu ya polisi wetu, utendaji wao na hata manung’uniko yaliyokuwepo hapo awali, kwa kiasi kikubwa yamepungua. Hongereni sana, na hivi ndivyo Jeshi la Polisi linavyopaswa kuwa,” amesema Mhe. Rais.
Aidha, Mhe. Rais amewapongeza wahitimu wote kwa kupata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo muhimu, pamoja na kuhimili changamoto za miezi tisa ya mafunzo. “Najua miezi tisa haikuwa rahisi ilikuwa na raha zake lakini pia haikukosa changamoto. Hata hivyo mmekomaa, mmejifunza, mmeiva, na sasa mmehitimu. Hongereni sana,” amesema kwa kuwapongeza wahitimu.
Mhe rais amehimiza kuwa maarifa na stadi walizopata chuoni ziwe msingi wa utendaji wao kazini. “Mkayazingatie mliyofundishwa na kuyatekeleza kwa vitendo. Ninyi sasa ndio mnaokwenda kuwa wakuu wa intelejensia, wa Polisi Jamii, oparesheni mbalimbali, uchunguzi wa kisayansi wa jinai, usalama barabarani, wakuu wa vituo vya polisi, upelelezi wa wilaya, na wasaidizi wakuu wa idara na vitengo mbalimbali – ndani ya mikoa na hata makao makuu ya Polisi.”

Katika hafla hiyo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa agizo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha linaweka mipango madhubuti ya kudhibiti viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani, hasa kuelekea Uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Rais Samia pia alionya dhidi ya vitendo vya rushwa ndani ya Jeshi la Polisi, akisema vitendo hivyo vinadhalilisha heshima ya jeshi na kuvunja uaminifu kati ya polisi na wananchi. Amesisitiza umuhimu wa polisi kuzingatia wimbo wao wa maadili na kushirikiana kwa karibu na jamii pamoja na vyombo vingine vya ndani na nje ya nchi, hasa katika kukabiliana na vitisho vinavyotokana na uhalifu wa mtandao unaovuka mipaka.
Kuhusu usalama barabarani, Rais Samia ameonyesha kusikitishwa na ongezeko la ajali kati ya Januari na Aprili mwaka huu ambapo ajali 1,322 ziliripotiwa, zikisababisha vifo vya watu 1,275. Aliwataka askari wa usalama barabarani kuwa makini, wabunifu na waweke masharti madhubuti kwa madereva ili kupunguza uzembe unaosababisha ajali.
Akitaja mfano wa ajali mbaya iliyotokea mkoani Mbeya iliyosababisha vifo vya watu 28, Rais Samia amevitaka vyombo vya usalama kuweka mikakati mipya ya kudhibiti ajali na kuimarisha ukaguzi wa vyombo vya usafiri kwa lengo la kupunguza janga hili la taifa.

Pia, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kuunganisha mifumo ya Jeshi la Polisi na taasisi nyingine za serikali ikiwemo Mahakama, ili kurahisisha uendeshaji wa kesi na utoaji wa huduma kidijitali, hatua itakayopunguza gharama na mlundikano wa kesi mahakamani.
Aidha, amewataka polisi kushirikiana kwa karibu na taasisi zinazopambana na dawa za kulevya na kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kwa ajili ya kuboresha utoaji wa haki nchini. Amebainisha kuwa serikali inaelewa changamoto ndani ya Jeshi la Polisi na itaendelea kuboresha maslahi yao kadri bajeti itakavyoruhusu.
Maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan yanaonyesha dhamira thabiti ya serikali katika kuhakikisha usalama na amani vinaendelea kulindwa nchini. Jeshi la Polisi linatakiwa kuwa na nidhamu, uwajibikaji, na kuzingatia maadili katika kila hatua wanazochukua ili kuleta imani kwa wananchi. Kupitia ushirikiano na taasisi nyingine na kuzingatia maagizo haya, tunaweza kuona Tanzania ikielekea kwenye uchaguzi salama, huku changamoto kama rushwa na ajali barabarani zikidhibitiwa kwa ufanisi.





