RAIS SAMIA ACHANGIA MILIONI 100 KUSAIDIA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUMU BAGAMOYO.

Scroll Down To Discover
Font size:

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amelisifu Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa kuonesha mfano bora wa utumishi wa dini unaogusa maisha ya watu kwa vitendo. Mhe. Rais ametoa pongezi hizo tarehe 11 Juni 2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kituo cha Watoto Wenye Mahitaji Maalumu cha Kitopeni-Bagamoyo Diaconic Lutheran Centre.

Katika hotuba yake, Mhe. Rais alieleza kuwa huduma zinazotolewa na KKKT ni kielelezo cha mafundisho ya kidini yanayotekelezwa kwa matendo, ikiwemo kuwatunza na kuwahudumia watu wenye uhitaji maalumu.

“Nimevutiwa sana na maandiko yaliyosomwa na Baba Askofu, yanayosema: ‘Amin nawaambia, kadri mlivyomtendea mmoja wa hawa wadogo mlinitendea mimi’. Huu ndio msingi wa kazi hii ya kiroho kuwahudumia wale wanaohitaji msaada wa jamii,” amesema Mhe. Rais Samia.

Aidha, Mhe. Rais amesisitiza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuunga mkono juhudi za taasisi za dini katika maendeleo ya kijamii, hususan kwa makundi maalumu, na itaendelea kushirikiana na wadau hao katika kuhakikisha huduma hizi zinapatikana kwa wakati na kwa ubora unaostahili.

Katika kuthibitisha dhamira hiyo, Mhe. Rais Samia amechangia Shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, huku wasaidizi wake na yeye binafsi wakitoa mchango wa ziada wa Shilingi milioni 150.

Mhe, Rias amesisitiza pia umuhimu wa jamii kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalumu hawabaguliwi wala kutengwa, bali wanapewa fursa sawa za malezi, elimu, na maendeleo.

“Kanisa limeonesha mfano wa kweli wa huduma ya dini si tu kwa mahubiri, bali kwa matendo. Linawavika, linawalisha, linawatembelea wagonjwa na linawafariji wahitaji. Huu ndio utumishi wa dini tunaoutaka kama taifa,” aliongeza Rais Samia.

Vilevile, Rais Samia aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa, hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea katika Uchaguzi Mkuu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kanisa la KKKT, ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Dkt. Alex Malasusa, alieleza kuwa jumla ya Shilingi bilioni 6.5 zimekusanywa katika harambee hiyo, ikiwa ni pamoja na ahadi na fedha taslimu kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kilichopo Bagamoyo, mkoani Pwani.

Askofu Malasusa alibainisha kuwa kituo hicho kitahudumia watoto wote wenye changamoto za kiakili na kimwili bila kujali dini, asili au hali ya kifamilia. Aliwasihi wazazi na walezi kutoendelea kuwaficha watoto wenye mahitaji maalumu, bali wawapeleke katika vituo vinavyotoa huduma za kitaalamu ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea.

Katika harambee hiyo, taasisi mbalimbali za kifedha na mashirika ya umma walijitokeza kuunga mkono juhudi hizo, ambapo miongoni mwao ni:

- Benki ya CRDB – Shilingi milioni 100

- Benki ya NBC – Shilingi milioni 50

- Benki ya NMB – Shilingi milioni 50

- Mashirika ya Umma – Shilingi milioni 150

- Benki ya Maendeleo – Shilingi milioni 140

- Wizara ya Fedha – Shilingi milioni 10

- Prof. Kitila Mkumbo – Shilingi milioni 10

Serikali inatoa wito kwa Watanzania wote kuendeleza mshikamano na moyo wa kujitolea ili kuhakikisha kuwa watoto wenye mahitaji maalumu wanapata mazingira salama, yenye fursa za ukuaji na mafanikio.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook