Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameanza rasmi ziara ya siku sita mkoani Morogoro kuanzia leo Agosti 2 hadi Agosti 6, 2024. Ziara hii ililenga kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Morogoro kupitia kuzindua miradi mbalimbali na kutoa maelekezo muhimu kwa viongozi wa mkoa na wananchi kwa ujumla.
Dhamira ya Ziara.
Dhamira kuu ya ziara ya Mhe, Rais Samia mkoani Morogoro itajikita zaidi katika kukagua na kuhakikisha miradi ya maendeleo inaendelea kwa kasi na kwa ubora unaostahili. Kama tulivyoshuhudia Rais Samia akisistiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na wananchi katika kutekeleza miradi hii ili kuhakikisha manufaa yanawafikia watu wote.

Miradi na Maeneo Muhimu Katika Ziara ya Mhe Rais.
Kuboresha Sekta ya Afya:
Katika ziara yake mkoani Morogoro, Rais Samia Suluhu Hassan amezindua miradi mbalimbali na kuainisha mipango ya kuboresha huduma za afya. Moja ya mafanikio makubwa ni uzinduzi wa Hospitali ya Gairo, ambayo imejengwa kwa kutumia fedha za serikali na ina vifaa vya kisasa. Rais Samia ameeleza kuridhishwa na matumizi ya fedha pamoja na kazi iliyofanyika katika hospitali hiyo, akiwataka wananchi kuitunza ili iendelee kutoa huduma bora.
Aidha, Rais Samia ameweka msisitizo juu ya ugawaji mzuri wa watumishi wa afya katika maeneo yote ili kuboresha huduma za afya. Rais, ameelekeza halmashauri kuhakikisha kuwa watumishi walioajiriwa hivi karibuni wanagawanywa vizuri ili vituo vya afya na hospitali zote zipate madaktari na wauguzi. Maelekezo haya yametolewa alipokuwa akizungumza na wananchi Wilayani Kilosa, ambapo alisisitiza umuhimu wa kupanga watumishi kwa ufanisi kutokana na uchache wao.
Rais Samia, pia amekuwa na lengo la kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Mkoa wa Morogoro. Na katika ziara hii ya siku sita, tayari amesisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto za miundombinu, hususan barabara zilizoathiriwa na mvua kubwa za El-Nino. Huku malengo makubwa ikiwa ni kuona matokeo ya matumizi ya fedha za serikali katika miradi ya maendeleo.
Hizi hatua zote ni sehemu ya juhudi za Rais Samia kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na miundombinu imara, sambamba na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa wananchi wa Morogoro na maeneo mengine nchini.
Kuzindua Daraja la Berege:
Katika hatua nyingine, Mhe Rais akiwa katika Wilaya ya Kilosa, amezindua daraja jipya la Berege ambalo litasaidia kuunganisha wananchi na kurahisisha usafirishaji wa mazao kwa kutumia magari makubwa badala ya pikipiki. Daraja hili ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo na litasaidia kupunguza gharama za usafirishaji.
Kubadilisha Matumizi ya Majengo:
Jambo jingine ambalo limepatwa kushuhudiwa katika ziara ya Mhe Rais Samia, ni kuridhia ombi la kubadilisha majengo yaliyokuwa yakitumiwa na World Vision kuwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi. Hatua hii inalenga kuboresha elimu na mafunzo kwa wananchi wa Morogoro na mikoa jirani, hivyo kusaidia kuongeza ujuzi na maarifa kwa vijana na watu wazima.
Mipango ya Baadaye : Kuendeleza Miradi ya Miundombinu:
Rais Samia hakusita kamwe kuweka msisitizo mkubwa kwenye ujenzi na uboreshaji wa miundombinu kama barabara na madaraja. Hii ni katika kuhakikisha kuwa kuna unafuu wa usafiri na usafirishaji wa bidhaa na huduma, jambo ambalo litachochea ukuaji wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla hususani miundombinu ya mkoani Morogoro.
Kuimarisha Huduma za Kijamii:
Katika juhudi za kuboresha maisha ya wananchi mkoani Morogoro, Rais Samia amehimiza uboreshaji wa huduma za afya, elimu, na maji safi. Maagizo yake kwa viongozi wa mkoa ni kuhakikisha kuwa rasilimali zinazotengwa na serikali zinatumika ipasavyo na kwa manufaa ya wananchi.
Kusikiliza Kero za Wananchi.
Rais Samia pia ametenga muda wa kusikiliza na kujibu kero mbalimbali za wananchi katika ziara yake mkoani Morogoro. Ambapo amewahakikishia wananchi kuwa serikali yake itafanya kila iwezalo kutatua changamoto zinazowakabili, ikiwa ni pamoja na migogoro ya ardhi, upatikanaji wa huduma za msingi, na kuongeza fursa za ajira.
Hitimisho.
Ziara ya Rais Samia mkoani Morogoro bado inaendelea mpaka tarehe Agosti 6, lakini mpaka sasa imeonyesha dhamira ya dhati ya serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo na ustawi. Kupitia miradi mbalimbali iliyozinduliwa na maagizo yaliyotolewa, Rais Samia ameweka msingi imara kwa maendeleo endelevu katika mkoa wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla. Ni matumaini kuwa hatua hizi zitachochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
