RAIS SAMIA ASIFU MAGEUZI YA MASHIRIKA NA TAASISI ZA UMMA

Scroll Down To Discover
Font size:

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameeleza kuridhishwa kwake na maendeleo yanayoshuhudiwa katika mashirika na taasisi za umma, ambapo serikali imepokea gawio na michango yenye thamani ya Shilingi trilioni 1.28. Fedha hizo zimepatikana kupitia mashirika ya umma yaliyo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na kampuni ambazo serikali ina hisa chache.

Makusanyo haya yameongezeka kwa asilimia 68 kutoka mwaka uliopita, ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 616 kilikusanywa. Ongezeko hili limechangiwa na mwitikio chanya wa mashirika na taasisi mbalimbali katika kutekeleza maelekezo ya serikali ya kuongeza ufanisi na tija. Serikali imedhamiria kukuza uchumi wa taifa kupitia uwekezaji wa umma na mageuzi ya kiuendeshaji katika mashirika haya, ikilenga kuongeza mapato yasiyo ya kikodi.

Rais Samia amekumbusha kuwa alipokutana na taasisi hizi mwaka jana, alieleza matarajio ya serikali kuona taasisi hizo zinachangia kwa kiwango kikubwa katika kukuza uchumi wa taifa. Kuimarika kwa mashirika haya kutayawezesha kukopa kwa uhuru katika taasisi za fedha za kimataifa, hali itakayosaidia kujenga heshima ya taifa kimataifa na kupunguza mzigo wa deni kwa serikali.

Katika kuhakikisha uendelevu wa mafanikio haya, Rais Samia ameagiza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Wizara ya Mipango na Uwekezaji kuweka malengo mahsusi ya mapato kwa kila taasisi ya umma. Akisisitiza umuhimu wa kutumia mifumo ya TEHAMA kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi, sambamba na kuwajengea uwezo watumishi wa umma katika nyanja za kisasa na kuwapatia motisha stahiki.

Hata hivyo, ameeleza kuwa bado kiwango kilichokusanywa hakijafikia matarajio ya serikali, kwani lengo ni taasisi za umma kufikia angalau Shilingi trilioni 1.5 kwa mwaka ujao kupitia mapato yasiyo ya kikodi. Rais Samia ameweka wazi kuwa mageuzi ya kweli yanahitaji ubunifu na taasisi kujitegemea katika kutatua changamoto zao bila kusubiri msaada wa serikali kila wakati.

Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amebainisha kuwa idadi ya taasisi zilizotoa gawio imeongezeka hadi kufikia 213 kutoka taasisi 145 mwaka jana. Kampuni zinazofanya biashara pekee zilitowa gawio la Shilingi bilioni 603.4. Hata hivyo, ameeleza kuwa mashirika 57 bado hayajatoa gawio, huku matarajio yakiwa ni kuongeza makusanyo kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha.

“Tunahitaji viongozi wanaogombea kwa kutumikia watu, si kwa misingi ya urafiki au kupewa nafasi. Mtu akiwa na kasoro, asemewe mapema. Hatutakubali nafasi za wananchi zigeuzwe miliki ya wachache,” alisisitiza.Rais Samia pia amehimiza mafunzo na maandalizi ya kina kwa wagombea wote, akibainisha kuwa mafanikio ya utekelezaji wa ilani hayawezi kufikiwa bila viongozi waliotayari na walioiva kisiasa na kitaaluma.

Mchechu ameeleza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya msukumo wa Rais Samia tangu hafla ya mwaka jana, ambapo alitoa maelekezo yaliyosisitiza kuongeza tija na ufanisi. Mchechu amesema kuwa safari ya mageuzi ya mashirika ya umma inadhihirika kupitia kaulimbiu ya mwaka huu inayosisitiza wajibu wa mashirika kuchangia maendeleo ya taifa kwa kuwa serikali sasa ni mwekezaji mkuu badala ya kuwa mtoa huduma pekee.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesisitiza kuwa mashirika ya umma ni chombo muhimu katika utekelezaji wa ajenda za maendeleo. Ametolea mfano wa mashirika kama TANESCO, TPA na TRC ambayo huchangia moja kwa moja katika ujenzi wa miundombinu ya nchi kama barabara, reli, na nishati.

Miongoni mwa taasisi zilizofanya vizuri ni Benki ya NMB ambayo imetoa gawio la Shilingi bilioni 68.1 kwa serikali mwaka huu, likiwa ni ongezeko kubwa kutoka bilioni 16.5 mwaka 2014. Aidha, kampuni ya Airtel Tanzania nayo imetoa mchango mkubwa wa zaidi ya Shilingi bilioni 739 na imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa tangu mwaka 2019 kupitia Airtel Money na Airtel Tanzania Plc, ambapo serikali inamiliki asilimia 49 ya hisa.

Utoaji wa gawio kutoka taasisi hizi unaonesha mafanikio ya dhahiri ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, na namna ambavyo mashirika ya umma yanavyoendelea kuimarika kutokana na mwelekeo mpya wa mageuzi ulioasisiwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Serikali ina matumaini kuwa mwelekeo huu utaendelezwa ili kufikia azma ya kuongeza mapato, kuimarisha uchumi, na kupunguza utegemezi kwa mikopo ya nje.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook