Dodoma, Tanzania – Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha 2025 hadi 2030, ambayo ameilezea kama nyaraka makini, yenye mwelekeo wa ushindi na inayotekelezeka kwa vitendo.
Akizungumza jijini Dodoma katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa uliofanyika tarehe 29-30 Mei 2025, Rais Samia amesema ilani hiyo imeandaliwa kwa weledi mkubwa, ikishirikisha wananchi na wadau mbalimbali, huku ikiwa imejikita katika kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kati ya 2020 na 2025, na kuelekeza nguvu katika kujenga uchumi wa kisasa unaogusa maisha ya kila Mtanzania.
“Ilani hii imeshiba. Imebeba dira ya maendeleo tunayoyahitaji kama taifa. Tumeshirikisha wataalamu, taasisi za elimu, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na wananchi wenyewe. Na zaidi, imezingatia hali halisi ya uchumi na uwezo wa nchi,” alisema Rais Samia.
Rais Samia amesisitiza kuwa utekelezaji wa ilani hiyo utategemea amani, mshikamano na bidii ya kila Mtanzania awe ni mfanyabiashara, mkulima, mchimbaji, mjasiriamali au mtumishi wa umma. Amesema kuwa ilani hiyo si ya viongozi wa juu pekee, bali ni mali ya kila mwanachama wa CCM na Watanzania wote.

Katika kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa wa karibu zaidi na unaoendana na uhalisia wa kila mkoa, Rais Samia ameagiza kutengenezwa kwa vitabu maalum vya Ilani kwa kila mkoa, vitakavyoainisha yaliyotekelezwa na mipango ya kipindi kijacho. Vitabu hivyo vitakuwa mwongozo wa utekelezaji kwa ngazi ya mikoa na vitasaidia kufuatilia maendeleo kwa usahihi.
Aidha, katika hotuba hiyo, Rais Samia ameweka msisitizo mkubwa katika uchaguzi wa wagombea kwa Uchaguzi Mkuu ujao. Huku akielekeza kuwa mchakato wa kuwapata wagombea lazima uendeshwe kwa uwazi, weledi na uadilifu mkubwa, kwa kuhakikisha wanapatikana wale wenye uwezo, maadili na uelewa wa dhati kuhusu misingi ya chama na changamoto za wananchi.
“Tunahitaji viongozi wanaogombea kwa kutumikia watu, si kwa misingi ya urafiki au kupewa nafasi. Mtu akiwa na kasoro, asemewe mapema. Hatutakubali nafasi za wananchi zigeuzwe miliki ya wachache,” alisisitiza.Rais Samia pia amehimiza mafunzo na maandalizi ya kina kwa wagombea wote, akibainisha kuwa mafanikio ya utekelezaji wa ilani hayawezi kufikiwa bila viongozi waliotayari na walioiva kisiasa na kitaaluma.
Mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na wawakilishi wa vyama rafiki kutoka nje ya nchi, wanadiplomasia, na wawakilishi wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora). Na katika hotuba yake, Rais Samia pia ametangaza kuwa CCM inajipanga kujenga Makao Makuu mapya ya kisasa jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 50 ya chama hicho yatakayofanyika mwaka 2027.
Kwa ujumla, kupitia hotuba yake ya uzinduzi wa Ilani ya CCM 2025–2030, Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameweka msingi thabiti na wa kisasa wa mwelekeo wa taifa letu katika miaka mitano ijayo. Kupitia msisitizo wake JUU YA ushirikishwaji wa wananchi, uwazi wa kiuongozi, weledi katika utekelezaji, mshikamano wa kitaifa na uwajibikaji wa viongozi..
