Katika hatua ya kihistoria inayolenga kuimarisha ushawishi wa Tanzania katika medani ya kimataifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2024, tarehe 19 Mei 2024 jijini Dar es salaam. Sera hii mpya ni matokeo ya mapitio ya kina ya Sera ya awali ya mwaka 2001/2004, ikiwa ni jibu la mabadiliko ya haraka ya mazingira ya kimataifa, kikanda, na kitaifa.
Kupitia sera hii, Serikali inalenga kuhakikisha kuwa diplomasia ya nchi inajielekeza katika kuleta maendeleo ya kiuchumi, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kuendeleza Kiswahili, kushirikisha Watanzania waishio nje ya nchi, na kushughulikia masuala mtambuka kama mabadiliko ya tabianchi, jinsia, na haki za binadamu. Ambapo baadhi ya masuala yaliyoainishwa na kuelezewa kwa kina katika sera hiyo ni pamoja na,
Kuimarisha Ushirikiano na Dunia
Sera hii mpya ya mambo ya nje imeweka msingi wa kuendelea kujenga uhusiano wa karibu kati ya Tanzania na mataifa mengine mbalimbali duniani kupitia diplomasia ya pande mbili na ile ya pande nyingi. Sera imetoa msisitizo kuwa Tanzania itaendelea kushiriki kikamilifu katika mashirika ya kikanda na kimataifa kama Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Mataifa (UN), G20, BRICS, na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), huku ikitetea maslahi ya nchi na bara la Afrika kwa ujumla.
Diplomasia ya Kiuchumi
Diplomasia ya kiuchumi ni moja ya nguzo kuu katika sera mpya. Sera hii imebainisha kuwa Tanzania itaendelea kutumia jukwaa la diplomasia kuvutia wawekezaji wa kigeni, kukuza biashara ya nje, na kutafuta fursa za ajira kwa Watanzania katika nchi mbalimbali. Katika hilo, serikali imejipanga kuhakikisha mabalozi na balozi zetu duniani kote zinakuwa kitovu cha kutangaza fursa za kiuchumi zilizopo nchini, na kusaidia katika utafutaji wa masoko ya bidhaa na huduma za Kitanzania.

Kuhusiana na Diaspora
Kwa mara ya kwanza, sera hii imeweka bayana dhamira ya serikali kuwatambua na kuwatumia Watanzania waishio nje ya nchi kama sehemu muhimu ya maendeleo ya taifa. Mchakato wa kutunga Sheria ya Diaspora unaendelea, na utahakikisha Watanzania hao wanatambulika sambamba na uhusiano na nchi yao, huku wakipata fursa ya kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo, kuruhusiwa tena kumiliki ardhi, na kuwekeza nyumbani. Vilevile, serikali inalenga kuwa na takwimu sahihi kuhusu diaspora ili sera na mikakati yao iwekwe bayana kwa ajili ya kuonesha uhalisia.
Kuinua Kiswahili Kimataifa
Katika kutambua umuhimu wa utamaduni kama nyenzo ya diplomasia, sera mpya imeweka mkazo mkubwa katika kuendeleza na kutangaza lugha ya Kiswahili duniani. Tanzania inajivunia mafanikio ya hivi karibuni ambapo Umoja wa Mataifa umetangaza rasmi Julai 7 kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, tukio ambalo ni ushindi mkubwa kwa diplomasia ya utamaduni na lugha. Aidha Rais samia amewataka viongozi Kuendelea kukuza hadhi ya nchi yetu kwa utajiri wa utamaduni wetu, mila na ustaarabu wetu na lugha yetu adhimu ya Kiswahili vitumike kama nyenzo ya kujenga ya ushawishi ambao ni muhimu sana katika kupanua masoko ndani ya bara la Afrika na nje ya bara la Afrika.

Mambo Mtambuka: Mazingira, Jinsia na Haki
Sera hii mpya ya mwaka 2024 inatoa majibu ya changamoto za sasa kwa kuweka msisitizo katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi, usawa wa kijinsia, haki za binadamu, na utawala bora. Sera imebainisha bayana kuwa Tanzania itaendelea kushiriki katika majukwaa ya kimataifa yanayolenga kutafuta suluhisho la changamoto hizi na kuchukua hatua madhubuti nyumbani, ikijumuisha kuhamasisha matumizi ya nishati safi na ulinzi wa mazingira.
Mafanikio ya Kidiplomasia Chini ya Uongozi wa Rais Samia
Toka aingie madarakani mwaka 2021, Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha uongozi thabiti wa kidiplomasia. Akiwa amefanya ziara zaidi ya 45 nje ya nchi na kuwapokea viongozi 37 wa kimataifa, amefanikisha kusainiwa kwa mikataba mbalimbali ya kimkakati katika sekta za miundombinu, elimu, afya, teknolojia na uwekezaji. Vilevile, Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika juhudi za kulinda amani katika ukanda wa Afrika kupitia ushiriki wake katika migogoro ya DRC, Msumbiji, na maeneo mengine.
Misingi Kumi ya Sera Mpya
Sera ya Mambo ya Nje ya 2024 inasimama juu ya nguzo kumi ambazo ni:
- 1.Diplomasia ya kiuchumi
- 2.Diplomasia ya amani na usalama
- 3.Usimamizi wa mikataba ya kimataifa
- 4.Mahusiano ya pande mbili
- 5.Diplomasia ya Kiswahili
- 6.Uchumi wa buluu
- 7.Ushirikiano na diaspora
- 8.Haki za binadamu na utawala bora
- 9.Mabadiliko ya tabianchi
- 10.Uongozi wa maendeleo endelevu
HITIMISHO
Uzinduzi wa Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2024 ni uthibitisho wa dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kuwa Tanzania inasikika, inaheshimiwa, na inanufaika katika uhusiano wake na mataifa mengine. Ni sera inayoweka raia mbele, inayotazama dunia kwa mtazamo wa kisasa, na kutoa majibu kulingana na nyakati tulizopo.