Katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Waandishi wa Habari (Samia Kalamu Awards) iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewahimiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao kama nyenzo ya kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kuchochea maendeleo, hasa tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.
Akizungumza mbele ya wadau wa habari na viongozi mbali mbali wa serikali, Mhe. Rais Dkt Samia alieleza kuwa waandishi wana nafasi ya kipekee ya kulinda maslahi ya taifa kupitia uandishi wa taarifa sahihi, zenye kujenga na kuhamasisha umoja wa kitaifa. Alieleza kuwa taaluma ya habari inapokuwa na mwelekeo wa kuelimisha, kutatua changamoto, na kuibua fikra chanya, taifa hujengeka kwa misingi imara ya maarifa na maadili.
Rais pia aligusia mabadiliko yanayoendelea kushuhudiwa kwenye sekta ya habari, akitambua kuwa vyombo vingi sasa vinaelekeza nguvu kwenye taarifa zenye uchambuzi wa kina, badala ya habari za uchochezi au dhihaka zisizo na tija. Alisisitiza kuwa uandishi wa habari wa kizalendo ni ule unaochambua kwa kina, unaotoa suluhisho, na unaoelekeza jamii katika fikra za maendeleo.

Katika kipengele cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Rais alitambua mchango mkubwa wa sekta hiyo katika kusaidia upatikanaji wa taarifa za masoko, bei za bidhaa, na fursa za kiuchumi. Alielekeza kuwa waandishi wanapaswa kutumia teknolojia kwa uangalifu na weledi, wakihakikisha wanachotoa kwa umma ni taarifa sahihi na zilizochambuliwa vyema.
Vilevile, Rais Samia alisisitiza matumizi sahihi ya takwimu na lugha ya Kiswahili katika uandishi. Alielekeza kuwa taarifa za kiuchumi au maendeleo zisielezwe kwa ujumla bila vielelezo halisi, na Kiswahili kinapaswa kutumika kwa ufasaha, kina na kueleweka kwa kila Mtanzania.
Aidha, alikumbusha kuwa uhuru wa vyombo vya habari haumaanishi uhuru wa kutoa taarifa za kuvuruga amani au kukiuka maadili ya kitaifa. Badala yake, uhuru huo utumike kwa ushirikiano na taasisi za serikali katika kutoa habari zenye kuleta maendeleo kwa taifa.

Sambamba na hayo, Rais Samia alieleza kuwa dira ya Tanzania ni kufikia kuwa nchi ya uchumi wa juu ifikapo mwaka 2050, ili kufikia hapo inahitaji mabadiliko ya fikra na mitazamo. Alisema kuwa waandishi wa habari wana nafasi muhimu ya kusaidia jamii kuelewa ajenda hiyo na kuisukuma mbele kupitia taaluma yao.
Mwishoni, alilipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kuandaa tuzo hizo, na kuahidi kuwa ofisi yake itaendelea kutoa ushirikiano katika kuinua taaluma ya habari nchini.