20 JUL 2025

Rais Samia Aongeza Mshahara wa Kima cha Chini kwa Watumishi wa Umma kwa 35.1%

Scroll Down To Discover
Font size: 15px12px

Katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyo fanyika mkoani Singida, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza kuongeza mshahara wa kima cha chini kwa watumishi wa umma kutoka Shilingi 370,000 hadi Shilingi 500,000. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 35.1 na linatarajiwa kuanza kutumika rasmi kuanzia Julai mwaka huu.

Rais Samia pia ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuboresha ustawi wa wafanyakazi kwa kuzingatia ukuaji wa uchumi unaotokana na bidii na mchango wa wafanyakazi hao katika maendeleo ya taifa.

“Baada ya kuangalia hali ya uchumi ambayo imeimarika kutokana na jitihada zenu, nina furaha kutangaza ongezeko hili la mshahara wa kima cha chini kwa watumishi wa umma. Hili ni takwa la haki kwa wafanyakazi na ni ishara ya kuthamini mchango wao,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amefafanua kuwa ngazi nyingine za mishahara pia zitaendelea kuongezwa kwa kadri bajeti ya serikali inavyoruhusu. Amesisitiza kuwa nyongeza hiyo ni sehemu ya dhamira ya serikali yake kuendeleza mageuzi ya kiuchumi yanayolenga kumuwezesha Mtanzania wa kawaida.

Sekta Binafsi na Maslahi ya Wafanyakazi

Katika hotuba yake, Rais Samia ameeleza kuwa Bodi ya Mishahara inaendelea kufanya mapitio ya maslahi ya wafanyakazi wa sekta binafsi, huku akihimiza wizara husika, waajiri na vyama vya wafanyakazi kufanya majadiliano ya mikataba ya hali bora za kazi.

Amehimiza waajiri na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kuwajengea uelewa wanachama wao juu ya haki za wafanyakazi ikiwemo uhuru wa kujumuika na kushiriki majadiliano ya maslahi mahali pa kazi. Mhe Rais amesisitiza kuwa majadiliano hayo huchochea tija na uzalishaji unaosaidia maendeleo ya taifa.

Ushirikiano wa Serikali na Vyama vya Wafanyakazi

Rais Samia pia ameitaka TUCTA kuweka utaratibu wa kutatua migogoro ya vyama vya ndani ya shirikisho hilo, akibainisha kuwa migogoro hiyo hupunguza ufanisi na uzalishaji. Amesisitiza umuhimu wa uwazi katika mapato na matumizi ya fedha za wanachama ili kuimarisha mshikamano na kuondoa ushawishi wa wanachama kujitoa kwenye vyama vyao.

Ajira zenye Staha na Bima kwa Wastaafu

Kuhusu changamoto za ajira katika sekta binafsi, Rais Samia amesema serikali inachukua hatua za kusimamia ajira za muda mfupi ili kuhakikisha zinazingatia haki na staha kwa wafanyakazi wote.

Vilevile, amewasihi wastaafu wa sekta binafsi kujiunga na huduma za bima ya afya kupitia Mfuko wa Bima ya Taifa (NHIF) na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF iliyoboreshwa), huku serikali ikiendelea kuboresha mfumo wa bima ya afya kwa wote, kwa kuwatambua wananchi wasio na uwezo na kuandaa vifurushi vya gharama nafuu.

Hitimisho

Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuthibitisha dhamira ya serikali ya awamu ya sita katika kuinua maisha ya wafanyakazi na kukuza uchumi jumuishi. Kupitia nyongeza ya mshahara wa kima cha chini, maboresho ya ajira, na juhudi za kupanua huduma za bima ya afya, serikali inaonesha wazi kuwa ustawi wa mwananchi ni kiini cha ajenda ya maendeleo.

or

For faster login or register use your social account.

Connect with Facebook