Dodoma – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt, Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 28 Aprili 2025, ameongoza hafla ya uzinduzi wa Benki ya Ushirika Tanzania (Coop Bank) ambapo katika uzinduzi huo amesisitiza umuhimu wa benki hiyo kuwa injini ya mapinduzi katika sekta ya ushirika na kuwawezesha wakulima kiuchumi.
Akizungumza katika tukio hilo, Rais Samia amesema benki hiyo imekuja katika wakati muhimu kwa wakulima, kwani itawawezesha kupata mitaji kwa ajili ya kuwekeza katika kilimo na kuimarisha upatikanaji wa masoko kwa mazao yao. Mhe, Rais ametoa wito kwa vyama vya ushirika kote nchini kushirikiana kwa karibu na benki hiyo ili kupanua huduma kwa maeneo mengi zaidi nchini.
"Kasi ya kuongezeka kwa mitaji katika kilimo imekuwa ndogo ukilinganisha na sekta nyingine, uwepo wa benki hii kutaongeza upelekaji wa mitaji kwa wakulima na sekta nzima ya kilimo," amesema Rais Samia.
Sambamba na hilo, Dkt, Rais Samia ameonya kuwa licha ya malengo ya maendeleo yaliyoambatana na kuanzishwa kwa Coop Bank, benki hiyo bado inapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya kisheria kama taasisi nyingine za fedha zinazosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Akiwahutubia wadau wa sekta ya fedha, Rais Samia pia ametoa rai kwa benki nyingine nchini kuiona Coop Bank kama mshirika wa maendeleo badala ya mshindani.
"Tushirikiane nayo, tufanye kazi nayo, najua biashara ya benki ni ushindani tunaweza kushindana nayo lakini kubwa tusaidiane nayo ili Watanzania waweze kunufaika na tuliyoyakusudia," amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Bank, Godfrey Ng’urah, amesema kuzinduliwa kwa benki hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, inayolenga kukuza sekta za uzalishaji na kuimarisha ushirika.
Ng’urah ameeleza kuwa Coop Bank ilianzishwa baada ya changamoto za ukwasi zilizozikumba Benki za Ushirika za Kilimanjaro na Tandahimba kati ya mwaka 2014 hadi 2020. Serikali iliona haja ya kuwa na benki imara ya ushirika, ambapo juhudi za awali ziliasisiwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, hayati Anna Mghwira.
Benki ya Ushirika inaanza kazi rasmi ikiwa na mtaji wa shilingi bilioni 58 na inamilikiwa kwa muundo ufuatao: asilimia 51 na vyama vya ushirika, asilimia 20 na Benki ya CRDB, asilimia 10 na Serikali, huku asilimia 9 ikimilikiwa na wawekezaji wengine. Awamu ya kwanza ya huduma za benki hiyo imejikita katika matawi manne yaliyopo Dodoma, Tabora, Kilimanjaro, na Mtwara, huku mawakala 58 kutoka vyama vya ushirika na Saccos mbalimbali wakisaidia kufikisha huduma kwa wakulima.

Ng’urah pia ametangaza kuwa tayari benki hiyo imesaini makubaliano na Bodi ya Stakabadhi Ghalani, pamoja na kuanzisha programu maalum inayolenga kurahisisha upatikanaji wa fedha kwa wakulima baada ya kuuza mazao yao.
Katika hotuba yake, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Abdulmajid Nsekela, amesema hatua zimechukuliwa kuunganisha vyama vya ushirika katika mifumo ya kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma, hatua inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta hiyo.
Akitoa hotuba yake Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, amesema ushirika ni sera ya msingi ya Chama Cha Mapinduzi, urithi kutoka kwenye harakati za ukombozi wa Afrika.
Wasira amewahakikishia wananchi kuwa lengo la sera hiyo ni kumkomboa mkulima na kuweka msingi wa ukombozi wa kiuchumi, ambao unalenga kuhakikisha kila Mtanzania anaishi maisha bora zaidi kila siku. "Kazi hii inatimiza azimio la kuhakikisha kila mwananchi anaishi vizuri na wananchi waishi maisha ya leo mazuri kuliko ya jana," amesema.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Uvuvi na Biashara, Deodatus Mwanyika, amesema uzinduzi wa Coop Bank umefungua ukurasa mpya katika sekta ya kilimo nchini. Mwanyika pia ameomba endapo Waziri Bashe ataendelea kuwa katika serikali ijayo, aendelee kuongoza Wizara ya Kilimo kutokana na ufanisi aliouonesha.