Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Toleo la Sheria Zilizofanyiwa Urekebishaji la mwaka 2023, akieleza kuwa ni nyenzo muhimu ya kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka, kuziba mianya ya rushwa, na kuimarisha misingi ya haki, amani, na maendeleo ya kiuchumi.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyondaliwa Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa toleo hilo limejumuisha sheria kuu 446 zilizogawanywa katika juzuu 21, ikiwemo sheria mpya 171 zilizotungwa kati ya mwaka 2002 hadi 2023. Amebainisha kuwa kazi hiyo ni matokeo ya mshikamano na weledi mkubwa wa taasisi za kisheria nchini.
“Sheria ni kioo cha ustaarabu wa jamii. Bila sheria zilizo wazi na zinazofahamika, haki haiwezi kupatikana, na taifa haliwezi kuendelea kwa ufanisi,” amesema Rais Samia.
Aidha, ameeleza kuwa kukamilika kwa toleo hili kunarahisisha utoaji wa haki kwa wananchi, kusaidia mahakama kufanya maamuzi kwa ufanisi zaidi, na kujenga imani ya wawekezaji kwa mifumo ya kisheria nchini.

Rais Samia ameeleza kuwa kazi ya kuandaa toleo hili imefanyika kikamilifu kwa kutumia fedha za ndani kiasi cha Shilingi Bilioni 10, ikilinganishwa na mwaka 2002 ambapo Benki ya Dunia ilifadhili kazi hiyo na wataalamu kutoka nje walihusika. Mwaka huu, wataalamu wa ndani pekee ndio wamesimamia mchakato huo, ikiwa ni alama ya kujitegemea na uwezo wa kitaifa.
“Sheria hizi zimechapishwa hapa hapa nchini, kila kitu kimefanyika na wataalamu wa ndani. Hii ni fahari kubwa kwetu kama taifa,” amesisitiza Rais Samia.
Katika kuhakikisha wananchi wote wananufaika na marekebisho hayo, Rais Samia ameagiza sheria hizo zifanyiwe tafsiri kwa Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kuelewa na kuzitumia kikamilifu katika maisha ya kila siku.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutumia fedha za ndani kuandaa toleo hilo na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya kujenga taifa imara lenye mifumo bora ya kisheria.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Hamza Johari, ameeleza kuwa toleo hilo limekusudia kurahisisha upatikanaji, usomwaji na utumiaji wa sheria hizo kwa wananchi, huku akibainisha kuwa marekebisho 1,039 yamefanyika katika kipindi cha miaka 21.
“Toleo hili linaonesha jinsi tulivyokomaa kama taifa katika usimamizi wa sheria zetu. Ni msingi wa kujenga jamii inayotambua haki na wajibu wake,” ameeleza Dkt. Johari.

Serikali pia imewekeza katika kuimarisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuanzisha Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, na kuongeza idadi ya mawakili wa serikali zaidi ya 50 ili kuendeleza maboresho haya kwa muda unaoendana na mabadiliko ya jamii.