Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inajulikana kama taasisi huru ya umma iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 1966, taasisi hii imeendelea kuimarika kama mhimili wa uthabiti wa sera za kifedha nchini.
Majukumu yake ya msingi inajumuisha kusimamia utekelezaji wa sera ya fedha, kusimamia sekta ya fedha, kuimarisha mifumo ya malipo, na kutoa ushauri wa kiuchumi kwa Serikali, mpaka sasa Benki Kuu imekuwa na mchango wa moja kwa moja katika kukuza uchumi wa taifa, na Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, taasisi hii imefanikisha mageuzi makubwa yaliyolenga kuimarisha uthabiti wa kifedha, kukuza uchumi shindani, na kujenga mazingira wezeshi ya kifedha kwa wananchi.
Katika kipindi hiki, mwenendo wa uchumi wa Taifa umeendelea kuimarika, ambapo Pato la Taifa limeshuhudia ongezeko la kasi ya ukuaji kutoka asilimia 4.8 mwaka 2020 hadi asilimia 5.1 mwaka 2023, licha ya changamoto za nje ya nchi ikiwemo majanga ya kiuchumi duniani.
Aidha, BoT imefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei kwa kiwango cha kuridhisha, ukishuka kutoka asilimia 3.1 mwaka 2020 hadi asilimia 3.0 mwaka 2024, hali iliyochangia kuimarisha ununuzi wa bidhaa na huduma na kuleta utulivu wa soko la fedha. Kwa upande mwingine, pato la ndani la Taifa limeendelea kupanuka kutoka shilingi trilioni 139.54 hadi trilioni 154.81 ndani ya kipindi hicho, huku msingi wa kodi ukipanuka kwa kuongeza idadi ya walipa kodi kutoka milioni 3.5 hadi milioni 6.4, na hivyo kuendelea kupanua shughuli za uchumi.

Katika maboresho ya utekelezaji wa sera za fedha, Januari 2024 BoT ilizindua matumizi ya Riba ya Benki Kuu (Central Bank Rate - CBR) kama chombo kikuu cha uelekezaji wa sera ya fedha, ikibadilisha mfumo wa awali wa udhibiti wa ujazi wa fedha. Maboresho haya yameongeza ufanisi katika kudhibiti mfumuko wa bei, kuweka mazingira ya kiuchumi yanayotarajiwa, na kuimarisha uwezo wa usimamizi wa sera za fedha kwa mujibu wa miongozo ya kimataifa.
Katika hatua nyingine, Sekta ya fedha imeonyesha maendeleo chanya ambapo akiba ya fedha za kigeni imeimarika na kufikia dola za Marekani bilioni 5.84 kufikia Desemba 2024, kiwango hicho kinajitosheleza mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kwa zaidi ya miezi 4.8, hivyo imeimarisha uthabiti wa urari wa malipo wa Taifa.
Sambamba na hilo, mauzo ya bidhaa nje ya nchi yameongezeka kutoka dola bilioni 8.81 mwaka 2020 hadi dola bilioni 14.66 mwaka 2024, hatua inayodhihirisha matokeo chanya ya juhudi za kupanua masoko ya nje na kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa.
Katika kulinda thamani ya mali za Taifa, BoT imeanzisha mkakati wa ununuzi wa dhahabu kwa ajili ya akiba, ambapo zaidi ya tani 3 zimekusanywa tangu mwaka 2023, na lengo ni kufikisha tani 6, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa kiuchumi.
Katika kuendeleza mifumo ya malipo ya kisasa na jumuishi, Benki Kuu ilizindua mfumo wa Tanzania Instant Payment System (TIPS) mwaka 2024, unaowezesha miamala ya papo kwa papo kati ya taasisi za fedha, bila kusahau Uboreshaji wa Mfumo wa TISS (Tanzania Interbank Settlement System) ambao umefungua fursa za kufanya miamala ya kuvuka mipaka kwa haraka na kwa ufanisi.

Tukizungumzia upande wa Huduma jumuishi za kifedha, huku nako kumeimarishwa kwa kiwango kikubwa, ambapo idadi ya kampuni za teknolojia ya fedha (Fintech) zilizosajiliwa imeongezeka kutoka 25 mwaka 2020 hadi 61 mwaka 2024, huku watumiaji wa huduma za malipo ya kidijitali wakifikia milioni 1.33.
Upatikanaji wa huduma za kifedha ndani ya umbali wa kilomita 5 umeongezeka hadi asilimia 89 ya wananchi, na pengo la kijinsia katika upatikanaji wa huduma hizo limepungua kutoka asilimia 10 mwaka 2017 hadi asilimia 3.6 mwaka 2023, hatua inayoweka Tanzania katika njia sahihi ya kujenga uchumi jumuishi unaompa nafasi kila mwananchi.
Kwa ujumla, mafanikio haya ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha uthabiti wa kiuchumi, kukuza ujumuishaji wa wananchi katika mfumo rasmi wa kifedha, na kuboresha nafasi ya Tanzania katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa kama nchi yenye uchumi unaokua kwa kasi, unaoweka msingi imara kwa maendeleo endelevu