Kwa mara ya kwanza Tanzania inashuhudia mageuzi makubwa katika kilele cha maonyesho ya kimataifa ya Nane Nane. Sambamba na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (MB), Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Maabara Kuu ya Kilimo inayojengwa Mji wa Serikali
Hatua hii ni ishara thabiti ya kujenga msingi imara wa sayansi na teknolojia katika sekta ya kilimo, ili kuleta mapinduzi yatakayowafaidisha wakulima wetu na kuleta maendeleo ya kweli kwenye kilimo nchini.

Jengo hilo la Maabara ya Kilimo lina ghorofa nne, na ndani yake zitakuwepo maabara takribani 14 ambazo zitawawezesha wataalamu na watafiti nchini kufanya tafiti za kina, zenye lengo la kuendeleza na kuboresha kilimo
Kwa kuweka jiwe hili la msingi, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha dhamira yake ya dhati ya kuifanya Tanzania kuwa kiongozi wa kilimo cha kisasa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara. Maabara hii ni muhimu kwa kuleta teknolojia mpya na mbinu bora za kilimo ambazo zitawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kufikia masoko ya kimataifa.
Kupitia juhudi hizi, serikali inazidi kuimarisha sekta ya kilimo, ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa letu. Wakulima wa Tanzania sasa wanaweza kuangalia mbele kwa matumaini zaidi, wakifahamu kuwa serikali yao inawaunga mkono kikamilifu katika safari ya kujiletea maendeleo endelevu kupitia kilimo.
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan pia ametembelea mabanda mbali mbali ya maonyesho, ambapo alipata fursa ya kujionea bidhaa na teknolojia mbalimbali zinazohusiana na kilimo. Aidha, amegawa tuzo kwa washindi mbali mbali waliojidhihirisha katika sekta ya kilimo, kama sehemu ya kutambua na kuhamasisha juhudi zao.
Kwa kuongeza, Mhe. Rais ameongoza makabidhiano ya Zana za Kilimo, ikiwemo Matrekta 519, Power Tiller 800, na Majembe ya kulimia 200, ambayo yataleta mabadiliko makubwa katika kuboresha uzalishaji wa kilimo nchini. Hii ni hatua nyingine muhimu katika kuhakikisha wakulima wetu wanapata nyenzo bora za kisasa za kuwasaidia kuongeza tija na kuboresha maisha yao.
