Kwa kutambua kuwa Vijana ndio nguzo ya maendeleo ya baadaye. Katika kuelekea kwenye uchumi wa kisasa, Tanzania inahitaji nguvu kazi yenye elimu, maadili na ujuzi wa kisasa. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kutambua umuhimu wa kuwaandaa vijana kupitia uwekezaji wa kimkakati katika sekta muhimu zinazohusu elimu, kilimo, biashara, na uwekezaji, ili kujenga taifa imara linalotazama mbele. Mfano ametekeleza yafuatayo:
1. Kipaumbele kwa Vijana katika Uongozi
Rais Samia ameweka msingi wa kuwaingiza vijana katika nafasi za uongozi. Kwa sasa ukitazama, vijana wengi wanashikilia nyadhifa za wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, na nafasi mbalimbali za utendaji serikalini. Hii ni ishara ya matumaini kwa vijana wanaotaka kushiriki kikamilifu katika kujenga taifa lao kwa mawazo mapya, kasi ya kiutendaji, na ari ya kuleta mabadiliko. Katika hafla moja ya kuapishwa viongozi, Rais Samia alitaja kuwa asilimia kubwa ya baraza lake ni vijana, akitoa mfano kuwa suruali za vijana zinabana zaidi kuliko za wazee — ishara kuwa vijana wana nguvu ya kuchapa kazi.
2. Uwezeshaji wa Elimu kwa Vijana
Ili kufanikisha azma ya serikali ya kuwa na kizazi chenye maarifa na ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira, Rais Samia ameiwezesha sekta ya elimu kwa kuimarisha mfuko wa mikopo ya elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB). Kwa mwaka 2024 pekee, serikali imeongeza bajeti hadi shilingi trilioni 1.98 kwa mikopo ya wanafunzi wa kada mbali mbali wa elimu ya juu. Pia, Rais mwenyewe amejitolea kutoa ufadhili maalum kwa vijana wa masomo ya sayansi na udaktari bingwa 1,109, akilenga kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa juu.
Kwa kuwekeza katika elimu, Rais Samia anajenga msingi wa taifa linaloongozwa na wataalamu wazalendo, walioelimika na wenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.

3. Kuendeleza Kilimo, Mifugo na Uvuvi
Kama tunavyofahamu kuwa Kilimo ni uti wa mgongo wa Tanzania, na Rais Samia amekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza sekta hii. Akiendelea na falsafa ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais Samia ameongeza bajeti ya kilimo, ambapo serikali imetenga shilingi trilioni 1.24 kwa mwaka 2024/2025 ili kuimarisha sekta hiyo. Lengo ni kuongeza uzalishaji na kuleta mapinduzi ya kijani. Amefanya uwekezaji mkubwa katika utafiti wa mbegu bora, ruzuku ya pembejeo, na miradi ya kilimo inayosimamiwa na vijana. Aidha, ametoa mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana wanaojihusisha na kilimo na uvuvi kupitia programu ya "Jenga Kesho Iliyo Bora."
4. Ajira na Uwekezaji kwa Vijana
Ili kupunguza tatizo la ajira, Rais Samia amewakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, akitambua kuwa uwekezaji unaleta ajira nyingi kwa vijana. Kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), miradi ya uwekezaji imeongezeka, na kufikia thamani ya dola bilioni 1.61 kwa robo ya mwaka wa mwisho, kiwango ambacho kinatoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa vijana. Katika ziara zake nje ya nchi, Rais Samia amekuwa akiwakaribisha wawekezaji na kuhamasisha diaspora kuja kuwekeza Tanzania ili kusaidia kutengeneza fursa za ajira na kuendeleza uchumi wa taifa.
5. Mikopo na Uwezeshaji wa Biashara kwa Vijana
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia pia imeanzisha Mpango wa Mikopo ya Samia, ukilenga kuwawezesha vijana, wanawake, walemavu, na makundi mengine maalum. Mikopo hii, yenye masharti nafuu, inalenga kuwapa vijana mtaji wa kuanzisha biashara zao. Serikali pia imetoa maelekezo kwa benki mbalimbali nchini kupunguza riba kwa ajili ya vijana wanaotaka kukopa na kuanzisha biashara zao.
Pamoja na mikakati ya mikopo, Rais Samia amewahimiza vijana kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Novemba 2024, ikiwa ni sehemu ya kujenga uzoefu na kuendeleza uongozi unaotokana na nguvu za vijana.

Hitimisho
Kwa kujitolea kuwekeza katika elimu, kilimo, biashara, na ajira kwa vijana, Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha kuwa na dhamira ya dhati katika kujenga taifa lenye nguvu kazi ya vijana wanaozingatia maadili, elimu, na weledi. Ni mpango unaolenga si tu kuendeleza taifa, bali pia kuwapa vijana nafasi ya kujijenga na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Tanzania. Rais Samia ameweka msingi wa taifa linaloongozwa na vijana wenye nia na uwezo wa kuleta mabadiliko chanya, hatua inayobeba matumaini makubwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.