Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kusimamia kwa kasi utekelezaji wa miradi 77 ya ujenzi wa barabara na madaraja nchini kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Miradi hii yenye thamani ya takribani Shilingi Trilioni 4.6 inalenga kuboresha mtandao wa barabara nchini na kurahisisha usafiri na usafirishaji.
Katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia, tayari TANROADS imekamilisha miradi 25 ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 1,198, mradi ambao umegharimu Shilingi Trilioni 1.68. Haya yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta, wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma (Dodoma Outer Ring Road) sehemu ya pili inayoanzia Ihumwa Dry Port, Matumbulu hadi Nala, kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 60.
Eng. Besta alieleza kuwa tangu Rais Samia aingie madarakani, ameweka kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja, jambo lililochochea kasi ya utekelezaji wa miradi muhimu kwa maendeleo ya taifa. "Hakuna mradi uliokwama kwa sababu Serikali inajitahidi kulipa wakandarasi kwa wakati kulingana na mikataba, jambo linalowezesha kazi kufanyika kwa ufanisi," alisema Besta.
Mafanikio ya Ujenzi wa Miundombinu ya Barabara.
Kwa mujibu wa Eng. Besta, Serikali tayari imelipa Shilingi Bilioni 101.1 kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi 24 ya barabara, sambamba na miradi minne (4) ya ujenzi wa viwanja vya ndege nchini. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Daraja la J.P. Magufuli (maarufu kama Kigongo-Busisi), ambalo linagharimu Shilingi Bilioni 717 na limekamilika kwa zaidi ya asilimia 94. Daraja hili linatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuchochea shughuli za uchumi na usafiri kati ya Mwanza na Geita.

Tanzania Kupanda Nafasi Afrika kwa Miundombinu Bora ya Barabara
Mafanikio haya ya ujenzi wa barabara na madaraja yameifanya Tanzania kupanda nafasi hadi ya 6 kati ya nchi 54 za Afrika zenye mtandao bora wa barabara, ikipanda kutoka nafasi ya 16 iliyokuwa mwaka 2022, kwa mujibu wa Takwimu za Statista.com. Hii ni ishara ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha miundombinu ya usafiri na kurahisisha shughuli za kiuchumi nchini.
Kwa kasi hii, Serikali ya Awamu ya Sita inaonesha dhamira ya dhati katika kuimarisha miundombinu, hali inayosaidia kuimarisha uchumi na kuvutia wawekezaji, pamoja na kurahisisha usafiri kwa wananchi.
