Serikali ya awamu ya sita imesaini mikataba mitano itakayowezesha kuanza ujenzi wa madaraja 13 katika sehemu za barabara zilizoathiriwa na Mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya katika Mkoa wa Lindi ambapo jumla ya Shilingi Bilioni 140 zitatumika katika utekelezaji huo.
Akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini mikataba hiyo Wilayani Kilwa Mkoani Lindi tarehe Oktoba 07, 2024, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua ukubwa wa athari ya miundombinu ya madaraja na makalvati katika Mkoa wa Lindi na kutenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kurudisha upya miundombinu hiyo.

Amesema ujenzi wa madaraja hayo utatekelezwa katika barabara kuu ya Malendego – Nangurukuru – Lindi – Mingoyo na barabara za Mkoa za Nangurukuru – Liwale, Kiranjeranje – Namichiga, Liwale – Nachingwea na barabara ya Tingi – Chumo – Kipatimu.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali ipo katua za mwisho za kusaini mkataba na Mkandarasi kwa ajili ya kujenga upya barabara ya Mtwara - Lindi - Pwani hadi Dar es Salaam ambapo utekelezaji utaanza awamu ya kwanza kuanzia Mtwara - Mingoyo na baadaye kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya awamu ya pili kuanzia Mingoyo hadi Dar - es Salaam.
Ujenzi wa madaraja 13 yatatekelezwa kwa muda wa Miezi 10 kwa kufuata taratibu zote za kitaalam na kusimamiwa na Kitengo cha TECU kutoka kwa Wakala huo.
#DiraYaSamia
